Simon Msuva amefuzu majaribio ya wiki moja kwenye klabu ya Bidvest Wits ya Afrika kusini na ameitaka klabu yake ya Yanga kutaja kiasi kidogo cha fedha ili aweze kujiunga nayo.
Msuva aliyetoa mchango mkubwa kwa Yanga hadi ikatwaa ubingwa wa ligi ya Vodacom msimu huu ikiwemo yeye kuibuka mfungaji bora ameiambia Kandanda anataka kwenda kutafuta changamoto mpya baada ya kuipa mafanikio timu yake ambayo ameichezea kwa moyo wake wote tangu alipojiunga nayo misimu miwili iliyopita akitokea Moro United.
“Nimemaliza kazi yangu ya majaribio na nadhani kila kitu kimekwenda sawa na jamaa wapo tayari kunisajili ninachoimba timu yangu Yanga kutaja bei ndogo ili niweze kucheza ligi ya Afrika Kusini msimu ujao kwa sababu haya nikama maisha kwangu japo naheshimu maneno ya viongozi wangu wa timu ninayochezea kwa sasa na bado nina mkataba nayo wa mwaka mmoja,”amesema Msuva.
Wits iko tayari kutumia dola 100,000 Sh. Milioni 200 kukamilisha dili zima la mchezaji huyo- kwa maana ya malipo ya mchezaji kusaini na ada ya uhamisho kwa klabu yake.