Tuesday, May 12, 2015

MSUVA MAMBO SAFI AFRIKA KUSINI, YANGA WALETEWA OFA RASMI YA KUMUUZA

MFUNGAJI bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Simon Msuva anarejea jioni ya leo Dar es Salaam na tabasamu ‘kuubwa’ baada ya kufaulu majaribio ya kucheza soka ya kulipwa Afrika Kusini.

Winga huyo wa mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga SC jana amekamilisha majaribio yake ya siku tatu Bidvest Wits ya Ligi Kuu nchini humo na matokeo ni ‘safi’.

BIN ZUBEIRY inafahamu Bidvest Wits wameridhika na uwezo Msuva na sasa wanafungua majadiliano na klabu yake, Yanga SC.

Msuva amebakiza mwaka mmoja katika Mkataba wake Yanga SC na Wits iko tayari kutumia si zaidi ya dola za Kimarekani 100,000 (Sh. Milioni 200) kukamilisha dili zima la mchezaji huyo- kwa maana ya malipo ya mchezaji kusaini na ada ya uhamisho kwa klabu yake.

Msuva aliondoka Dar es Salaam Jumatano wiki hii akiwa tayari ameipa Yanga SC ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu, huku pia akiwa anaongoza kwa mabao, 17 akifuatiwa na mchezaji mwenzake wa timu hiyo, Amissi Tambwe mabao 14. - Amekosa mechi mbili za mwisho dhidi ya Azam FC Yanga ikilala 2-1 na leo dhidi ya Ndanda ya Mtwara.

Tangu ajiunge na Yanga SC mwaka 2012 akitokea Moro United, Msuva ameifungia timu hiyo mabao 35 jumla katika mechi 102 za mashindano yote.

Chanzo: BinZubeiry Blog