PC Gineneko akiwa na majeraha baada ya kuvamiwa na majambazi. Watekaji hao mara baada ya kumpora bunduki askari huyo eneo la Yombo, Ilala jijini Dar es Salaam walitoweka kusikojulikana.Habari kutoka eneo la tukio zinasema kuwa watekaji hao idadi yao inakisiwa kuwa sita na walijiandaa kufanya tukio hilo kutokana na mazingira yalivyokuwa. Haruni Sanchawa na Shani Ramadhani
Askari Polisi wa Kikosi cha Tazara jijini Dar es Salaam kinachosimamia ulinzi na usalama wa Reli ya Tanzania na Zambia aliyetajwa kwa jina la PC Gineneko, ametekwa kisha kuporwa bunduki aina ya SMG ikiwa na risasi 30 , Mei 27, mwaka huu.
Shuhuda aliyesimulia tukio hilo huku akiomba jila lake kuhifadhiwa kwa sababu za kiusalama, alisema ilikuwa saa 12 jioni ambapo askari huyo alikuwa katika majukumu yake ya ulinzi na wenzake na walipofika kwenye baa moja (jina linahifadhiwa) walimkuta kijana anafanya biashara ya kuuza CD.
“Yule kijana mwenye CD akaanza kuzozana na mwenzake, mmoja akadai kuwa amekuwa akimwibia CD zake na kwenda kuuza sehemu nyingine, askari baada ya kuona mzozo umekuwa mkubwa walikwenda kuwahoji kisa cha kugombana.
“Wakati vijana wale wakiendelea kuhojiwa na askari, walitokea watu sita bila kujua walikuwa na lengo gani, wakasema wanamtaka muuza CD , kabla polisi hawajakaa sawa, vijana wale waliwazingira askari akiwemo aliyekuwa na bunduki ghafla wakaanza kumshambulia kwa kumkata kwa panga na kumpora bunduki aina ya SMG iliyokuwa na risasi 30 na kutomea.
Mfano wa bunduki aina ya SMG aliyoporwa. Mmoja wa maafisa wa polisi ambaye si msemaji, aliliambia gazeti hili kuwa mbinu waliyotumika majambazi wale ni mzozo ulioanzishwa na wauza CD, hivyo kufanikisha tukio la uporaji silaha.Katika tukio lingeni, jeshi la polisi kikosi hicho cha Tazara wakati linasaka silaha hiyo, Juni 9, mwaka huu lilifanikiwa kukamata bunduki nyingine maeneo ya Kwa Ally Mbowa baada ya kuwashitukia majambazi watatu waliokuwa kwenye pikipiki.
“Askari wa doria (maarufu kama tigo) walifanikiwa kuwadhibiti majambazi hao, mmoja alikamatwa na wananchi wenye hasira wakampiga hadi kufa lakini bunduki aina ya AK 47 iliyokuwa na risasi 13 ilipatikana,” alisema afisa huyo.
Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Reli, Tazara, SACP Patrick Byatao hakupatikana kufafanua matukio hayo licha ya kutafutwa kwa njia ya simu.