Msanii wa filamu Bongo, Fatuma Ayubu `Bozi’ akihamisha vitu vyake.
Msanii wa filamu Bongo, Fatuma Ayubu `Bozi’ amejikuta akifungasha virago na kuhama kwenye nyumba aliyokuwa akiishi maeneo ya Kinondoni jijini Dar kutokana na mjengo huo kutawaliwa na mauzauza yanayosadikiwa kuwa ya kishirikina.
Chanzo makini kilicho jirani na nyumba aliyokuwa akiishi mwanadada huyo kilieleza kuwa, baada ya kuvumilia vimbwanga vya kishirikina ameamua kuondoka.
“Hii nyumba wapangaji huwa hawadumu kwa kushindwa kustahimili wanayoyaona sijui ina balaa gani, tunashangaa yeye ameweza kukaa kwa mwaka mzima na kuvumilia majanga yote, inataka moyo.
“Sasa leo uzalendo umemshinda baada ya mpangaji mwenziye kufariki ghafla wiki iliyopita, ambapo siku moja kabla ya kifo chake alipambana na paka aliyekojoa mlangoni, tangu itokee hiyo ishu amekuwa akija hapo kuchungulia nyumba na kuondoka, leo kaona isiwe tabu, anahamisha vitu vyake,” kilisema chanzo.
Baada ya kupata fununu hizo bila kupoteza muda wadakuzi wetu waliibuka nyumbani kwa msanii huyo na kumkuta akiwa kwenye hekaheka ya kuhama na kukiri kuwa amelazimika kufanya hivyo kutokana na aliyokuwa akiyaona kwenye nyumba hiyo.
“Kuna muda nikiwa chumbani nasikia taa zinawashwa na kuzimwa nikitazama sioni mtu, wakati mwingine paka anakuja chumbani na kucheza kwenye kioo ukimfukuza na kufunga mlango dakika chache unamuona tena na cha kustaajabisha nakuwa najiuliza amepita wapi sipati jibu, kwa ujumla nyumba hii ina mauzauza kibao ambayo nimeshindwa kuyavumilia, hali ni mbaya nahamia kwa rafiki yangu,” alisema Bozi.