Tuesday, June 16, 2015

MAKAVU LIVE: KWA NINI UACHWE WEWE KILA SIKU?

 
Mungu ni mwema! Leo kama ada tunakutana mpenzi msomaji wangu wa Love & Life katika kilinge chetu hiki kwa lengo la kuelimishana na kukumbushana masuala ya mahusiano ambayo yametawala kwa kiasi kikubwa maisha yetu.Leo tutazungumzia kuhusu tatizo linaloonekana kukithiri na kuwatatiza watu wengi ambao wamejaribu kuingia kwenye uhusiano wa mapenzi na kujikuta wakiambulia maumivu ya kuachwa kila mara na watu waliowakabidhi mioyo yao wakiamini wataishi pamoja mpaka kifo kuwatenganisha.
Tukubaliane kwamba, kutendwa au kuachwa kwenye mapenzi ni jambo la kawaida. Watu wengi wamewahi kuachwa na wapenzi wao na katika hali nyingine watu haohao waliotendwa huweza kuwaacha wapenzi wengine waliowapenda; yote hii ni kawaida, lakini hali hii huwa tatizo pale ambapo mtu anayeachwa au kuumizwa anakuwa ni yuleyule.
Mpenzi msomaji wangu, ni kweli kwamba tatizo hilo halijali mwonekano mzuri wa mtu au usiovutia, huweza kumtokea mtu yeyote na wakati wowote ule.
Swali la kujiuliza ni kwamba, kwa nini inatokea kwako kila mara? Nani mwenye tatizo, wewe au wapenzi unaokutana nao? Ukiweza kujiuliza na kupata ufumbuzi katika maswali hayo hakika utapata jawabu la jambo hili.
Tukumbuke kwamba, kuachwa au kutendwa muda mwingine huweza kusababisha matatizo makubwa ikiwa muhusika amekabidhi asilimia kubwa ya moyo wake kwa yule aliyenaye kwenye mahusiano.Mfano; mtu anaweza kujiingiza kwenye masuala ya ulevi uliokithiri, utumwa wa mapenzi, kujiua au kuua na matatizo mengine ya kisaikolojia.
Nikwambie tu kwamba, tatizo hili halihitaji mganga wa kienyeji kulitatua, dokta au mchungaji kukuombea. Kikubwa unatakiwa kufahamu mambo kadhaa ambayo kimantiki yanaweza kukusaidia ukadumisha uhusiano wako na kuepukana na tatizo hili.

Fahamu, amekupendea nini?
Hili ni jambo kubwa na lenye maana kufahamu kama kweli unahitaji kudumu katika uhusiano wako. Suala hili halijalishi kuwa wewe ni mwanamke au mwanaume, ni wajibu wa wote kufahamu uliye naye anavutiwa na wewe kwa sababu gani.
Huenda alikupenda kwa sababu wakati mnakutana ulikuwa ni mweusi unayeng’aa lakini baadaye mkumbo wa ulimbukeni wa kuendana na wakati ukakupitia hatimaye ukakuzoa kiasi cha kuanza kujibadilisha ngozi, maumbile na vitu vingine.Kitu kidogo kwenye mahusiano kinaweza kusababisha madhara makubwa sana!
Je, tabia zako zinaridhisha?
Usijifungie chumbani na kulia siku nzima au wiki huku ukihisi ukiwa mkuu kuwa wewe ni mtu mwenye mkosi usiye na thamani duniani.
Ili kumaliza tatizo la kukimbiwa na wapenzi unao anzisha nao mahusiano tumia muda mwingi kujipeleleza juu ya tabia ulizo nazo kuwa zinaridhisha au la!Ikiwa ngumu kwako mwenyewe kugundua uzuri au ubaya wa tabia zako, fanya upelelezi kwa kuwatumia marafiki na watu wako wa karibu, inaweza kukusaidia pia kumaliza tatizo lako.
Wapo watu wanawakwaza wenzi wao kwa sababu ya kupenda kunung’unika kupita kiasi, kusema uongo, ulevi na mambo mengine ambayo awali hawakuwanayo.Mbaya zaidi wenzi wao wanapohoji kuhusu tabia hizo, huwa wakali jambo ambalo siyo zuri.

Ukweli ni kwamba, sababu zipo nyingi sana za mtu kutodumu katika ndoa au uhusiano anao anzisha, jambo la msingi si kutumia muda mwingi kulaumu bali tumia muda mwingi kujiuliza unakosea wapi na rekebisha makosa.
Tukutane wiki ijayo kwenye mada nyingine nzuri.