Friday, June 5, 2015

MASTAA NA UPEPO WA KISIASA BONGO!!!

Na Hamida Hassan
Kuanzia Jumamosi iliyopita, viongozi mbalimbali wamekuwa wakijitokeza na kutangaza nia ya kugombea nafasi ya urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).Hakika idadi ni kubwa lakini mwisho wa siku lazima apatikane mmoja ambaye atachuana na mgombea kutoka Ukawa.
Rose Ndauka.
Kutokana na hilo, mastaa wa hapa Bongo nao wamekuwa sehemu ya kutangaza nia kwa waheshimwa hao kwani wapo walioonesha wazi kuwa wanamuunga mkono nani huku wengine wakibaki na siri moyoni.Mwandishi wa makala haya amejaribu kuzungumza na baadhi ya mastaa hao kujua wako upande gani na wanazungumziaje upepo wa kisiasa kwa sasa.
Wastara Juma
Kiukweli sipendi sana mambo ya siasa lakini linapokuja hili la watangaza nia ya kugombea urais, naomba niseme tu kwamba nataka kuongozwa na mtu ambaye hatakuwa na tamaa ya kujinufaisha yeye.
 Awe ni kiongozi asiyekuwa na njaa ambaye akiingia ikulu hataangalia tumbo lake na watu wake wa karibu bali kushughulikia matatizo ya wananchi.
Rose Ndauka
Ninaye ambaye ningependa awe rais wa nchi hii lakini kwa sasa siwezi kumuweka wazi. Hata hivyo, natamani apatikane mtu mwenye nia ya dhati ya kuiongoza nchi hii kwa haki.
Maimartha Jesse.
Maimartha Jesse
Mimi bwana ni Team Lowassa! Sababu ya kumuunga mkono kiongozi huyu ni kwamba, anajitambua na ni mtu anayeweza kuchukua maamuzi magumu.Mimi nina imani naye na naamini akipewa nafasi ya kuingia ikulu, mambo mengi yatakuwa sawa likiwemo hili la elimu ambalo limekuwa ni kipaumbele chake.
Miriam Jolwa - Kabula
Kwenye hili la urais nawaunga mkono watu wawili, kati yao akipita mmoja itakuwa poa tu. Kwanza ni Makongoro Nyerere ambaye ni mtu wa nyumbani lakini pia Lowassa ambaye licha ya mimi kumkubali pia anaonekana kukubalika kwa wananchi.
Ester Kiama.
Ester Kiama
Mchuano kwa sasa uko kwa Membe na Lowassa. Wote ni viongozi wenye sifa ya kuliongoza taifa hili vizuri tu.
Lakini sasa ukiniambia nichague mmoja nitasema Lowassa. Unajua kwa nini? Ni mtu ambaye amejitosheleza, hana shida kiasi kwamba hata akiingia pale ikulu hataanza kwanza kujikusanyia mali na fedha.
Kulwa Kikumba ‘Dude’
Mimi huniambii kitu kwa Lowassa. Ni mtu makini, ana nia thabiti ya kuliongoza taifa hili lenye matatizo kibao.
Halima Yahya ‘Davina’
Mimi siyo mshabiki wa mambo ya siasa na ndiyo maana hata upepo unavyokwenda mimi naona sawa tu. Ila kwa uzalendo lazima nitapiga kura na kiongozi atakayepitishwa na Chama Cha Mapinduzi basi nitampigia kura.
Mbali na mastaa hao waliojaribu kuweka wazi hisia zao, wengine walionekana kuchenga na kutotaka kusema wapo upande gani. Mastaa hao ni pamoja na Elizabeth Michael ‘Lulu’, Blandina Chagula ‘Johari’ Jacqueline Wolper, Jokate Mwegelo na Mahsein Awadh ‘Dk. Chen’.