Mbunge wa Mbeya Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mheshimiwa Joseph Mbilinyi ‘Sugu akiwa na mwanaye.
BAADA ya Mbunge wa Mbeya Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mheshimiwa Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ kuripotiwa kumfikisha mahakamani mzazi mwenziye, Faiza Ally, Juni 19, mwaka huu akitaka mahakama impe haki ya kumlea mtoto wao, Sasha (2), sakata limeisha kwa Sugu kukabidhiwa mtoto amlee.
Katika hukumu ya kesi hiyo iliyosomwa juzi Jumanne huku upande wa mlalamikaji ambaye ni Mhe. Sugu ukiwakilishwa na mwanasheria wake kutokana na Sugu kuwa bungeni mjini Dodoma, mdaiwa Faiza alionekana kubanwa na baadhi ya vielelezo huku suala la maadili likiwa ndiyo sababu kuu ya kumkosesha haki ya kumlea mtoto huyo.
HUKUMU ILIVYOTOLEWA
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mfawidhi Patrick Vaginga wa Mahakama ya Mwanzo Manzese/Sina jijini Dar, alisema baada ya kupitia maelezo ya pande zote mbili, yaani mlalamikaji ambaye ni Sugu na mlalamikiwa ambaye ni Faiza, mahakama hiyo imempa Sugu haki ya malezi ya mtoto kutokana na upungufu wa malezi ya mama ambaye ni Faiza.
FAIZA AKIRI
Hakimu Vaginga alisema kuwa kutokana na mlalamikiwa kukiri vielelezo vyote vya picha za nusu utupu ambavyo mlalamikaji, Sugu aliviwasilisha dhidi yake, mahakama imeona kumwacha mtoto kwa mama kutaathiri makuzi kwa kuwa mtoto hujifunza haraka akiwa katika umri huo hasa kupitia mama.
VILIVYOMPONZA FAIZA
Hakimu huyo alivitaja baadhi ya vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo na Sugu kuwa ni picha ya Faiza akiwa amevaa pampasi.
Picha hiyo ilipigwa kwenye ‘bethidei’ yake, Desemba 18, mwaka jana. Picha akiwa amevaa shati tu ambayo alipigwa kwenye shoo ya Zari iliyojulikana kwa jina la Zari All White Party iliyofanyika Mei Mosi, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar.
Hakimu Vaginga aliitaja picha nyingine kuwa ni ile ya kigauni kifupi kilichoacha makalio nje. Alipigwa kwenye hafla ya Tuzo za Kili Music iliyofanyika Juni 13, mwaka huu katika Ukumbi wa Mlimani City.
FAIZA AANGUA KILIO MBELE YA HAKIMU
Mara baada ya hukumu hiyo kusomwa, Faiza alishindwa kujizuia na kuangusha kilio mfululizo mbele ya hakimu, ikabidi atoke nje akisindikizwa na askari ili kuwezesha mahakama kuendelea na kesi nyingine.
FAIZA BAADA YA KUNYAMAZA KULIA
Baadaye akiwa ameacha kulia, waandishi wetu walimfuata Faiza akiwa ndani ya gari na kumuuliza alivyojisikia kufuatia hukumu hiyo, akasema:
“Siwezi kusema lolote lakini Mungu anajua. Mimi siwezi kuishi bila mwanangu Sasha. Nawaambia nitakufa. Sidhani kama wiki itapita mimi sijafa.”