Monday, June 22, 2015

MJUE BILIONEA ANAYETAKA KUINUNUA ARSENAL

Bilionea Aliko Dangote
LONDON, England
BILIONEA Aliko Dangote anataka kuinunua Arsenal. Mfanyabiashara huyu wa Nigeria, ndiye mtu mweusi namba mbili mwenye nguvu zaidi duniani, nyuma ya Rais wa Marekani, Barack Obama na ana fedha mara mbili zaidi ya mmiliki wa Chelsea, Mrusi Roman Abramovich.Dangote ndiye Mwafrika tajiri zaidi duniani na sasa amekuwa gumzo kwenye soka kutokana na dhamira yake ya kutaka kuinunua Arsenal.
Bilionea huyu anaweza akawa hafahamiki sana kwa mashabiki wa Uingereza, lakini ana fedha za kutosha kufanikisha ndoto zake za kuimiliki Arsenal.Kwa sasa tajiri Mmarekani Stan Kroenke ndiye mwenye hisa nyingi zaidi katika kikosi cha Arsenal akiwa hafikii hata nusu ya utajiri wa Dangote, akifuatiwa na Mrusi tajiri zaidi, Alisher Usmanov ambaye naye hafikii utajiri wa Dangote.
 ALIKO DANGOTE NI NANI?
Ni Mnigeria mwenye umri wa miaka 58 ambaye anamiliki viwanda vikubwa vya saruji, ngano na sukari. Dangote anasambaza asilimia 90 ya sukari kwa Wanigeria milioni 170, ikiwa ni idadi kubwa sana ya mauzo.
 Pia Dangote anajenga kiwanda kikubwa cha mafuta barani Afrika ambacho kinatarajiwa kukamilika mwaka 2018.
ANA UTAJIRI KIASI GANI?
Jarida maarufu la Forbes linamtaja kama tajiri namba 67 duniani, akiwa na utajiri wa zaidi ya pauni bilioni 12 (zaidi ya Sh trilioni 42). Kama akiinunua Arsenal, utajiri huo utamfanya awe mmiliki tajiri zaidi kwenye Ligi Kuu England, mara mbili zaidi ya Abramovich ambaye ni namba 137 duniani. Dangote anatokea katika familia ya wafanyabiashara matajiri katika Jiji la Kano, mjomba wake alimpa mkopo akiwa na umri wa miaka 21 kwa ajili ya kuanzisha biashara zake mwenyewe.
 JE, YEYE NI MTU MUHIMU?
Uchunguzi wa Forbes umebaini kuwa yeye ni mtu mweusi namba mbili mwenye nguvu zaidi duniani nyuma ya Obama. Ni mtu mwenye ushawishi mkubwa zaidi Afrika na hata Obama alihakikisha anaonana naye alipokuwa akihutubia Soweto mwaka 2013. Marekani inapoandaa mipango ya biashara na ya kupambana na ugaidi Afrika, Dangote ni mmoja wa watu wa kwanza kutafutwa.
 KWA NINI ARSENAL?
Alipokuwa bilionea wa kawaida, Dangote alijaribu kununua asilimia 15 za hisa za Arsenal kutoka kwa mwanadada Nina Bracewell-Smith, ambaye baadaye aliziuza kwa Kroenke, lakini sasa kwa kuwa amekuwa tajiri mkubwa zaidi, anataka aimiliki timu hiyo yeye mwenyewe.
 STAILI YA MAISHA YAKE IKOJE?
Anaishi katika Kisiwa cha Victoria ambacho ni cha watu matajiri jijini Lagos. Anaishi kwenye jumba kubwa ambalo lina mionzi ya kuzuia risasi kwenye kila dirisha na ulinzi mkali. Ni Muislam. Alisomea biashara katika Chuo Kikuu cha Cairo, Misri na ana watoto watatu. Ana sifa ya utanashati na huwa anaachia mustachi.
 NIGERIA WAMPONDA KUITAKA ARSENAL
Ligi ya Nigeria inahitaji miundombinu mizuri ili kuendelea kuwatunza wachezaji wazuri, hivyo Wanigeria wanaona siyo sawa Dangote kukimbilia kuinunua klabu ya Ulaya, wakati alipaswa aanze kufadhili mpira wa nchini kwao.
 Kocha wa zamani, Mnigeria Adegboye Onigbinde, anasema: “Kwake kutoifikiria ligi ya kwetu inaonyesha picha mbaya. Ni bora kwake kusambaza fedha zake kwa hekima. Tunachohitaji zaidi kwenye nchi hii, ni mtu anayeweza kufadhili programu za chini kabisa.”
 ATAIPATA ARSENAL?
Inategemea jinsi Kroenke anavyofikiria. Maana Kroenke ni mtulivu mno na hupenda kuyatunza mawazo yake ndani ya nafsi yake. Hivi sasa Arsenal inaingiza fedha baada ya kujenga Uwanja wa Emirates, pengine Kroenke angependa apate faida japo kwa miaka mingine michache ijayo.
 NINI KINATARAJIWA KUTOKA KWA DANGOTE?
Dangote anatarajiwa kumwaga fedha kwa mchezaji yeyote yule anayemtaka, kwa kuwa ana fedha za kutosha, hivyo kuifanya Arsenal iwe kubwa zaidi Ulaya na duniani. Alishasema atahitaji mataji, hivyo kocha Arsene Wenger atatakiwa kubadilisha falsafa yake ya kutegemea zaidi makinda.