Friday, June 19, 2015

‘Ukimwi Unawamaliza Vijana wa Miaka 10-24’


SERIKALI imesema  vijana nchini wenye umri kati ya miaka 10 hadi 24 wanakabiliwa na janga la taifa la maambukizi ya virusi Ukimwi , mimba za utoto na vifo vinavyotokea wakati wa kujifungua kitendo ambacho kinadhoofisha nguvu kazi kazi  ya maendeleo ya taifa.
 
Imesema vijana ambao ni tegemeo kubwa la taifa lakini wamejiingiza katika ngono  zembe  na kuoa au kuolewa wakiwa katika umri mdogo jambo ambalo limesababisha  kundi hilo kuishi na maambukizi ya virusi vya Ukimwi na vifo wakati wa kujifungua.
 
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Dk. Faisal Issa, alikuwa akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano wa uhamasishaji juu ya afya ya uzazi na maendeleo ya vijana.
 
Alisema vijana walio na umri katia ya miaka 10 hadi 24 wapo katika kipindi cha mabadiliko ya saikolojia na mwili.
 
Dk. Issa alisema takwimu  za sensa ya 2012 zinaonyesha vijana nchini  ni zaidi ya asilimia  31 ambapo kundi  hilo lipo katika hatari ya kukumbwa na matatizo ya afya ya uzazi, magonjwa ya kuambukizwa kwa nia ya ngono.
 
“Kiwango cha vifo vya wanawake vinavyotokana na matatizo ya uzazi kitaifa ni 454 kwa kila vizazi hao 100,000. Mimba katika umri mdogo huchangia mara mbili hadi tano ya vifo.
 
“Kwa Mkoa wa Mwanza   akina mama waliohudhuria kliniki ni 131,536 lakini kati ya hao 27,727 ni vijana wa chini ya umi wa miaka 20 ambao ni asilimia 21.
 
“Kiwango cha vifo vya wanawake vitokanavyo na uzani ni 112 kwa kila vizazi hao 100,000 kwa mwaka 2010 lakini mwaka 2014,   vifo 113 vilitokea kati ya vifo hao 100,000 ambapo kati ya hivyo vifo 40 vilikuwa kwa upande wa vijana chini ya miaka 24 ambayo ni asiliamia 35,”alisema.
 
 Alisema kutokana na hali hiyo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Kitengo cha Afya ya Uzazi na Mtoto, kimeanzisha semina maalumu ya elimu kwa makundi hayo ili kubadili tabia na kupunguza maambukizo ya Ukimwi na vifo vya uzazi.