Wednesday, June 17, 2015

WACHEZAJI TAIFA STARS WASHUKA KWENYE BASI NA KUMPA KICHAPO SHABIKI ALIYEWATUPIA JIWE

WACHEZAJI wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars leo wamelazimika kuteremka kwenye basi lao makutano ya barabara za Msimbazi na Nyerere na kumpiga shabiki.
Hatua hiyo ilifuatia shabiki mmoja aliyekuwa kijiweni kutupia jiwe basi hilo wakati timu hiyo inatoka hoteli ya Tansoma, eneo la Gerezani, Dar es Salaam walipoweka kambi yao, kuelekea Uwanja wa Karume kwa mazoezi ya jioni.
Wachezaji walimuambia dereva asimamishe basi wakamshikishe adabu aliyepiga jiwe basi hilo- na dereva akafanya hivyo.
Hata hivyo, shabiki huyo hakupata ‘kichapo kikali’, kwani wasamaria wema walijtokeza kuwasihi wachezaji hao wamuache, nao wakarejea kwenye basi lao na kuendelea na safari.  
Kitimutimu; Wachezaji wa Taifa Stars wakimpa kibano shabiki

Hii inakuwa mara ya pili kwa basi hilo la Stars kupigwa mawe likiwa limebeba wachezaji, kwani juzi pia watu wasiojulikana walilishambulia kwa mawe basi hilo hadi kuvunja kioo cha dirisha moja eneo la Shaurimoyo.
Basi hilo lililokuwa limebeba baadhi ya wachezaji wa tumu hiyo waliokuwa wakitoka mazoezini Uwanja wa Karume, Dar es Salaam lilishambuliwa kwa mawe na watu wanaosadikiwa kuwa mashabiki wenye hasira baada ya matokeo mabaya mfululizo.
Jumapili Taifa Stars ilifungwa mabao 3-0 na Misri katika mechi yake ya kwanza ya Kundi G kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika 2017 mjini Alexandria.
Shabiki (kulia) aliyekula kibano baada ya kupiga jiwe basi la Stars akifarijiwa na wenzake
Wachezaji wa Stars wakiondoka kurejea kwenye basi lao

Mabao yote ya Misri yalipatikana kipindi cha pili, wafungaji Rabia dakika ya 61, Morsi dakika ya 65 na Mohamed Salah dakika ya 70.
Lakini wachezaji ambao walishambuliwa kwa mawe wakiwa kwenye basi hilo, hawakwenda Misri. Kikosi cha Stars kilichokuwa Misri, kiliwawasili jana na kuungana na wenzao waliobaki Dar es Salaam.
Kwa pamoja wachezaji hao watakwenda kambini Zanzibar kesho kwa maandalizi ya mchezo wa CHAN dhidi ya Uganda mwishoni mwa wiki.
Kipigo cha Misri kilikuwa cha nne mfululizo kwa Stars chini ya kocha wake, Mholanzi Mart Nooij baada ya awali kufungwa mechi zote tatu za Kundi B Kombe la COSAFA mwezi uliopita 1-0 na Swaziland, 2-0 na Madagascar na 1-0 na Lesotho mjini Rusternburg Afrika Kusini.
Kwa ujumla huo unakuwa mchezo wa 17 kwa Nooij tangu aanze kuinoa Taifa Stars Aprili mwaka jana akirithi mikoba ya Mdenmark, Kim Poulsen kati ya hizo akiwa ameshinda mechi tatu tu.
Leo imekuwa mara ya pili basi la Taifa Stars kupigwa mawe na mashabiki