Ukijaribu kufuatilia utabaini kuwa, wengi ambao sasa ni maarufu, wamefanya mambo makubwa! Walikuwa hawajulikana huko nyuma lakini walipoingia kwenye muziki, filamu na fani nyinginezo kisha wakafanya vizuri, walijikuta kwenye orodha ya mastaa.
Kwa hapa Bongo, wapo watu ambao wana majina lakini yawezekana wasingeingia kwenye uhusiano wa kimapenzi na wale ambao tayari ni mastaa, wasingekuwa na umaarufu walionao leo.
Ezden Jumanne
Huyu fani yake ni ya utangazaji. Kwa wale wanaofuatilia mambo watakumbuka kuwa, kabla ya kuanzisha uhusianao na mtangazaji mwenzake Khadija Shaibu ‘Dida’, hakuwa maarufu.
Walipoanzisha uhusiano ndiyo habari zake na mpenzi wake huyo zikaanza kuandikwa na kujikuta akijulikana sana. Hata hivyo, utakubaliana na mimi kwamba, tangu ndoa yao ivunjike, kama vile ameanza kufifia hivi licha ya kuwa bado anaendelea kufanya vizuri kwenye utangazaji wake kupitia TV One.
Siwema Edson
Ni binti wa mjini ambaye inadaiwa anafanya kazi kwenye shirika moja la ndege nchini. Licha ya vurugu zake alizokuwa akifanya mjini, hakuupata umaarufu, alipokuja kunasa kwenye penzi la mwanamuziki Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’ jina lake likaanza kupaa.
Penniel Mungilwa 'Penny'
Ni mtangazaji anayeimudu vyema fani hiyo lakini ni ukweli ulio wazi kwamba, kabla ya kuwa na uhusiano na Mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond’, hakuwa akujulikana kivile.
Baada ya kuanza kumuita msanii huyo baby…sweetheart, honey na majina mengine matam, akaanza kuwa staa. Ila, kuoneshwa kuwa alibebwa na Diamond, sasa hivi umaarufu wake umepungua tangu waachane.
Moze Iyobo
Dogo ni dansa wa Mwanamuziki Diamond. Alianza kufanya kazi hiyo muda mrefu lakini hakuwa maarufu. Jina lake likaanza kupaa baada ya kudaiwa kuwa anatoka na Aunt Ezekiel.
Baada ya kuvuma kwa tetesi hizo, wengi walishindwa kuamini kutokana na kwamba, wawili hao hawaendani. Jina likazidi kukua baada ya kuwepo kwa taarifa kwamba hata mimba ya Aunt ilikuwa ikimhusu.
Hapo ndipo kijana huyu akaanza kung’aa na kuwa maarufu kiasi kwamba sasa hivi huwezi kumtaja Aunt bila Moze.
Malick Bandawe
Ni mwanamuziki, mmoja kati ya waanzilishi wa Kundi la TNG lililokuwa na maskani yake jijini Tanga. Hakuwa maarufu kiivyo licha ya kwamba alikuwa akifanya vizuri kwenye muziki.
Alipozama kwenye penzi zito na msanii wa filamu, Rose Ndauka, mara nyingi alikuwa akiandikwa na kumfanya awe maarufu. Na yeye sasa hivi kama anapotea baada ya penzi lao kuvunjika.
Bond Suleiman
Fani yake ni utangazaji, anajihusisha pia na mambo ya filamu lakini baada ya kudaiwa kutoka na Lulu Semagongo kisha kuhamia kwa Wastara Juma, sasa hivi naye amekuwa staa.
Ni wazi kwamba, kama siyo Anti Lulu na Wastara, huenda angekuwa anajulikana lakini si kwa kiwango cha sasa.
Abdallah Mtoro ‘Dallas’
Ni mfanyabiashara ambaye alikuwa hajulikani kabisa. Upedeshee wake wa enzi hizo ukamkutanisha na msanii wa filamu, Jacqueline Wolper.
Baada ya wawili hao kuwa wapenzi, jina lake likawa maarufu lakini na yeye baada ya kuachana na Wolper kisha kudaiwa kufulia, umaarufu ‘kwishinei’.
Faiza Ally
Miongoni mwa mabinti mcharuko kwa sasa mjini, Faiza ni mmoja wao. Hakuwa na jina kabisa lakini alipodondokea mikononi mwa mwanasiasa Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, habari zao zikaanza kuandikwa.
Hata hivyo, hakuwa maarufu, aliuheshimu uhusiano wao, akaficha makucha. Walipoachana, Faiza akaanza kuonesha yeye ni nani.
Kila mtu sasa anamjua kutokana na tabia zake. Uvaaji wake wa kihasara ndiyo ambao kwa kiasi kikubwa umemfanya leo hii awe maarufu.
Zarinah Hassan ‘Zari’
Ni ukweli usiopingika kwamba, hapa Bongo mpenzi huyo wa Diamond hakuwa akijulikana sana. Alipowekeza penzi lake kwa staa huyu kutoka Tandale, vyombo vya habari vikaanza kumuandama.
Leo hii anaweza kuwa staa ambaye jina lake ni maarufu sana kuwashinda hata baadhi ya mastaa wa kike Bongo.