Wednesday, June 17, 2015
WEMA SEPETU JIFUNZE KUWEKA BREKI MDOMONI
Wema Isaac Sepetu ‘Madam’
SALAMU nyingi zikufikie mrembo usiyechuja umaarufu tangu mwaka 2006, Wema Isaac Sepetu ‘Madam’ vipi uko poa? Mishemishe zinakwendaje?
Ukitaka kujua afya yangu, mimi namshukuru Mungu kwani ni mzima, hofu na mashaka ni kwako wewe uliye mbali na upeo wa macho yangu. Kitambo kidogo kimepita sijakuona lakini naamini u-mzima wa afya.
Mbali na kukusalimia, dhumuni la barua hii ni kutaka kukumbusha juu ya umuhimu wa mdomo wako kuwa na staha. Kuna vitu vya kuzungumza lakini kuna ambavyo vinapaswa kuwekwa ‘spea’.
Binafsi sikufurahishwa na namna ambavyo ulimpa maneno makali aliyekuwa rafiki yako, Kajala Masanja kupitia kipindi cha televisheni wiki iliyopita.Si busara kumtusi mwenzako hadharani kiasi kile. Hata kama amekukosea kiasi gani, wewe ni mtu maarufu unapaswa kuhakikisha kile unachokizungumza kitakuwa na matokeo gani mbele ya jamii inayokuzunguka.
Ugomvi wenu wewe na Kajala una historia ndefu, kibusara hakukuwa na sababu ya kuendeleza mjadala ambao hata watu tayari walishaanza kuusahau. Vitabu vya dini vinatufundisha, kusamehe na kusahau.
Nilishawahi kukuandikia barua huko nyuma, nilikusihi usamehe hili suala liishe. Nilisema hivyo kwa sababu mara kadhaa Kajala ameshaonesha nia ya kutaka yaishe lakini wewe ukaendeleza vita. Kwa nini usimsamehe? Mbaya zaidi hata huyo mwanaume ambaye inasemekana alikuibia naye nimetonywa kuwa ameshaachana naye.
Nyinyi mlishibana kama marafiki wa kuambiana kila kitu, la kwako la Kajala na la Kajala la kwako watu wanashindwa kuwaelewa kama kweli mlishibana kwa nini msikae na kuanza ukurasa mpya?
Sijawahi kumsikia Kajala anakuzungumzia vibaya lakini wewe kila siku unamsema. Unafikiri yeye hana mabaya yako? Akiyaanika hadharani utafurahi? Haiwezi kuwa sawa.Nakulaumu wewe zaidi katika hili maana historia inaonesha haudumu na marafiki. Uliwahi kuwa na urafiki na kina Jack wa Chuz, Rose Ndauka, Jamila na wengine kibao lakini wote uliwaacha njiani.
Kama hiyo haitoshi, Aunt naye mmedumu kwenye ushosti kwa muda mrefu lakini naye pia miezi kadhaa iliyopita mlitofautiana na sina hakika kama hadi sasa mpo sawa kama zamani japo mlipatanishwa.
Nikusihi, badilika. Kuwa na staha, chunga sana kauli zako kwani wewe unaheshimika katika jamii.
Nikushukuru kwa kunisoma!
Mimi ni kaka yako,
Erick Evarist