Sunday, July 19, 2015

ACT NAKO KUMEKUCHA!!! MGOMBEA URAIS KUJULIKANA ,TAARIFA YAO IKO HAPA


CHAMA cha ACT Wazalendo leo kimetoa ratiba yao kwa wanahabari kuhusu kutangaza wagombea wake wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba 2015.


Ifuatayo ni taarifa yao kwa wanahabari:

Ndugu waandishi wa Habari
Karibuni kwa mara nyingine katika makao makuu ya Chama chetu.
ACT Wazalendo tunaendelea kuwashukuru kwa kuitikia wito wetu kila mara tunapowaita kwa ajili ya kuchukua habari na kuzifikisha kwa umaa, hili linatutia moyo na tunawashukuru sana

Ndugu Waandishi wa Habari
Tumewaiteni leo tukiwa na mambo Machache Muhimu kwa chama chetu na Taifa kwa ujumla ambayo tungependa mtusaidie kufikisha kwa umma.

Julai mosi mwaka huu Chama Cha ACT-Wazalendo kilifungua rasmi pazia la uchukuaji wa fomu za kugombea nafasi mbali mbali za uongozi, kwa ajili ya kuwawakilisha wananchi katika majukumu ya kiserikali.
Nafasi hizo ni kuanzia Udiwani Ubunge na Urais ambao kitaifa wawakilishi hao watapatikana Oktoba 25 baada ya kupigiwa kura na wananchi.


Ndugu waandishi wa habari
Tangu kuanza kwa uchukuaji huo wa fomu kumekuwa na mwitikio mkubwa wa wanachama wetu kuchukua fomu hizo. mapaka sasa kuna baadhi ya majimbo na kata zina watia azma kuanzia wanne mpaka tisa hili ni jambo la faraja kwetu.



Kati ya majimbo 265 yakiwamo majimbo mapya 26 yaliyoongezwa hivi karibuni na Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC), ACT-Wazalendo tumeshakuwa na waweka azma zaidi ya mmoja katika majimbo 226 kwa nchi nzima na tunaamini mpaka kufikia mwisho wa uchukuaji fomu ndani ya Chama majimbo yote 265 yatakuwa yanawatia azma mbali mbali wanaosubiri kupitishwa na chama kwa ajili ya uchaguzi mkuu.


Kichama mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu kwa nafasi ya udiwani ni julai 24, kwa nafasi ya Ubunge mwisho julai 31 na nafasi ya Urais mwisho wa kuchukua na kurudisha ni Agosti mosi.


Ndugu waandishi wa habari
Mwisho wa uchukuaji na urudishaji wa fomu hizo utafuatiwa na vikao mbali mbali vya uteuzi kwa ngazi husika kabla ya kufika katika ngazi ya Taifa.


Kwa ngazi ya Taifa Halmashauri kuu itakutana Agosti 13 kwa ajili ya kuteua jina la mgombea Urais wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, pamoja na kupendekeza majina ya wagombea Urais kwenye mkutano mkuu.


Agosti 13, Mkutano mkuu utamchagua mtu atakayepeperusha bendera ya Chama cha ACT Wazalendo katika mbio za urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Tarehe hizo pia zianaweza kusogezwa mbele kwa sababu maalum na uamuzi unaweza kufanywa Sekretariti ya Chama baada ya kukaimu baadhi ya majukumu ya kamati kuu

Ndugu waandishi wa habari.
Pamoja na mafanikio yote tunayopata ACT-Wazalendo lakini pia kuna watu bado wanatufanyia michezo michafu kwa kuwarubuni na kuwahadaa watu wetu waliotia azma ya kugombea nafasi mbali mbali hususan maeneo ambayo mawasiliano yana matatizo.


Hivi karibuni tumepokea taarifa kutoka katika miji ya Tarime na Rorya Mkoani Mara kuwa kuna watu wanapita na kutangaza kuwa Chama chetu kimezuiwa kushiriki Uchaguzi kwa muda wa miezi sita.


Tumebaini lengo la upotoshaji huu ni kuwakatisha watanzania tamaa juu ya ukuaji wa Chama Cha ACT-Wazalendo pamoja na dhamira yake nzuri ya kuirudisha nchi katika misingi iliyoachwa na hayati Mwalimu Julius Nyerere.


Tunawataarifu wananchi kuwa Chama chetu kitashiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu kwa kuweka wagombea wa nafasi zote na Chama hakitakuwa tayari kuona sehemu yoyote ya nchi mgombea wa CCM anapita bila kupingwa.


Ndugu waandishi wa habari.
Pia katika mkutano wetu wa leo tunapenda kuwatambulisha wanachama wetu wapya walio mbele yenu
Hawa ni Msanii maarufu wa filamu nchini Mohamed Mwikongi “Frank” na Mwingine ni Deo Meck
Deo Meck kabla ya kujiunga na ACT Wazalendo alikuwa mwenyekiti wa kitengo cha vijana Taifa wa NCCR Mageuzi.


Kwa pamoja hawa wameungana nasi kwa ajili ya kuendeleza uzalendo kwa Taifa lao nasi tunawakaribisha.
Pia tendo hili la leo la kuwakaribisha vijana hawa ni mwanzo wa kuwatambulisha wanachama mbali mbali wakiwemo wabunge na viongozi wa vyama waliojiunga nasi baada ya kuvunjwa kwa Bunge.


Tayari tunao baadhi ya watu waliokuwa wabunge na wameshajiunga nasi na mchakato wa kuwatambulisha unaendelea katika maeneo mbali mbali nchini.
Nawashukuru kwa kunisikiliza


Msafiri Mtemelwa
Naibu Katibu Mkuu,ACT Wazalendo
Julai 16/2015