Thursday, July 9, 2015

DODOMA SASA KUMEKUCHA, ASKARI WA KIKOSI CHA FARASI WATANDA BARA BARANI, ULINZI KILA KONA YA DODOMA


IKIWA imebaki siku tatu kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumpata mgombea wake Wajumbe wa Mkutano Mkuu zaidi ya 3,000 tayari wamewasili mjini Dodoma na kusababisha ulinzi mkali kuimarishwa kila kona ya mji huo.
Polisi waliovaa sare na wale wasiovaa sare wameonekana kila eneo la mji wa Dodoma wakiwemo wale wa Kikosi cha Farasi ikiwa katika kuhakikisha kuwa hali ya amani na utulivu inaendelea kuwepo kutokana na Serikali nzima kuhamia mji huo kwa ajili ya mchujo wa kumpata mgombea urais atakayepeperusha bendera ya CCM.

Kila kona ya mji wa Dodoma wananchi na baadhi ya wageni wamekuwa wakizungumzia mchakato huo ambao ni mgumu ndani ya CCM wa kuhakikisha kuwa wanampata mgombea ambaye anakubalika na kuuzika kwa wananchi.
Baadhi ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu huo ambao ndio watakaopitisha jina la mgombea urais wamesema ikiwa Kamati Kuu ya CCM itawapa jina la mgombea ambaye haendani na maisha ya Watanzania wamesema hawatapiga kura na kisha watatoka nje.

Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana wajumbe hao wamesema kwa sasa hata wao wamechoka kutokana na vitendo vinavyofanywa na baadhi ya wagombea ambapo baadhi yao walichukua takwimu za wanachama waliofariki na kudai kuwa wamepata wadhamini wengi.

Walisema ni bora Azimio la Arusha lirudi kwa muda lakini wanaitaka Kamati Kuu kufanya uamuzi sahihi katika kumpata mgombea urais wa CCM vinginevyo ni bora wasipige kura na kama itawezekana basi watalikataa jina la mgombea urais litakalopitishwa.

Wajumbe hao ambao hawakutaka kutaja majina yao walisema wanataka kiongozi wa leo kwani kila mtu anaitwa mzee akiwemo January Makamba, Mark Mwandosya na Makongoro Nyerere ambao wao kwa mtazamo wao wanaamini kuwa ndio wanaweza kuwapitisha mmoja kati ya hao.

Wakizungumzia kuhusu kupewa fedha na mmoja wa wagombea wa chama hicho ili wampitishe, walisema wao hawawezi kuhongwa kwa kuwa wako zaidi ya 1,900 sasa huyo ambaye anatajwa ana hela ya kuwahonga wajumbe wote atawezaje.

"Hatujui nani kahongwa kama ambavyo habari zimeenea lakini ukweli ni kwamba huyo anayetajwa kuwahonga sidhani kama anafedha ya kuwahonga wajumbe wote lakini sisi tunavyodhani inawezekana huyo aliyesambaza habari hizo ndiye anayehonga watu hao,"walisema wajumbe hao.

Kwa upande wake Kada anayedaiwa kutumika na mgombea nafasi ya Urais kugawa fedha Cyprian Musiba, alisema anashangazwa na tuhuma kuwa alikuwa akigawa fedha na kisha kukamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wakati jambo hilo sio na kweli.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana Musiba alisema hizo ni siasa chafu za kutaka kuwachafua watu ili waonekane kuwa ni watoa rushwa wakati wanaosambaza habari hizo ndio hao wahusika.

"Kama mnavyoniona hapa na mimi nimeita ili kuwaambia ukweli hivi kama ni kuwahonga unawahonga wajumbe wa Mkutano Mkuu wangapi jamani hata ninyi waandishi hebu pimeni wenyewe kweli kila mmoja apewe kiasi walichosema ni jambo la ajabu sana na ukweli ni kwamba hizo habari si za kweli,"alisema Musiba.

Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete jana alitarajiwa kuongoza kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili ya Chama hicho ambacho kilishindwa kuanza katika muda mwafaka kutokana na sababu ambazo hazikufahamika.

Kikao hicho ni moja kati ya vikao vitatu muhimu katika kuelekea kumpata mgombea wa chama hicho ambapo leo Rais Jakaya Kikwete atazindua ukumbi mpya wa CCM ulioko nje kidogo ya mji wa Dodoma kabla ya kwenda kulivunja Bunge na baadaye kuhudhuria Kikao cha Kamati Kuu ya CCM ambacho kitakuwa na majina matano ya awamu ya kwanza ya wagombea.