Mteule wa kuwania urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi katika Uchaguzi Mkuu ujao, John Pombe Magufuli na Katibu Mwenezi wa CCM, Nape NNauye wakipiga ngoma.
Mwandishi wetu
WAKATI mteule wa Chama Cha Mapinduzi katika Uchaguzi Mkuu ujao, John Pombe Magufuli akifahamika kama mtu makini kwenye utekelezaji wa majukumu yake, imethibitika kuwa waziri huyo wa Ujenzi pia ni mkali kwenye upigaji wa tumba, Risasi Jumamosi linakupa zaidi.
Hali hiyo imefahamika baada ya gazeti hili kuchimbua matukio mbalimbali ambayo yamemuonyesha mbunge huyo wa Chato akipiga tumba kwa umahiri mkubwa kiasi cha kuwaacha hoi watu wengi.
Mathalan, katika uzinduzi wa daraja la Mbutu, wilayani Nzega mkoa wa Tabora, uliofanyika Januari 7, 2013, Magufuli alionekana akipiga Tumba wakati bendi kongwe ya Msondo Ngoma ikitoa burudani katika hafla hiyo, akiwa sambamba na wanamuziki wa kundi hilo, Shaaban Dede na Hassan Moshi ‘TX Jr.
Licha ya siku hiyo, pia kwa nyakati tofauti Magufuli alionyesha umahiri wake katika kupiga Tumba katika hafla mbalimbali, kama vile wakati wa ziara ya Rais Jakaya Kikwete mkoani Kagera, alipojiunga na kundi la uhamasishaji na burudani la chama hicho tawala, kwa kukitendea haki kifaa hicho cha muziki.
Aidha, wabunge wawili wa upinzani, John Mnyika (Ubungo) na Halima Mdee wa Kawe, watakuwa ni mashuhuda wa uhodari wa Magufuli, kwani katika hafla ya uzinduzi wa barabara ya Msewe- Baruti iliyofanyika miezi michache iliyopita, mteuliwa huyo wa CCM aliifanya tena shughuli hiyo mbele ya umati wa wananchi waliohudhuria.
Aidha, hivi karibuni wakati akitambulishwa kwa wanachama wa chama hicho kama mgombea wake katika Viwanja vya Zakheem, Mbagala jijini Dar es Salaam, akiwa pamoja na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, Magufuli pia alipiga tumba kwa umahiri wa hali ya juu kabla ya kuhutubia mamia ya wanachama hao.
Mwanamuziki mmoja kutoka bendi moja kubwa nchini aliyeomba hifadhi ya jina lake, alisema Magufuli ni mkali na anaweza kuwafunika wapigaji tumba wengi nchini.
nn
bb
nn