WIKI iliyopita, tuliishia kwa kueleza jinsi alivyojitosa rasmi kwenye biashara ya kuuza nafaka za mahindi na mpunga akitoa katika mikoa ya Mbeya na Tanga. Tuliishia kwenye kipengele cha alipougua fangasi.
Je, nini kilifuata? Endelea sasa.
“Kilikuwa ni kipindi kigumu mno maishani mwangu, sikuwahi kuwaza hata siku moja kama ningekuja kuugua ugonjwa kama huo,” anasema JB.
“Basi, maisha yakasonga kama kawaida huku biashara nayo ikizidi kuimarika kwa kuniletea mafanikio mengi, lakini nikiwa katika kilele hicho cha mafanikio, mara nikaanza kukutana na ushawishi wa jambo ambalo sikuwahi kuwaza hata siku moja kama ningeweza kulifanya, jambo lenyewe ni kufanya maigizo,” anasema JB.
JB anasema mtu aliyeanza kumshawishi ajiingize kwenye mambo ya uigizaji ni msanii mwenzake, Single Mtambalike ‘Richie’. Hata hivyo msanii huyu anaweka wazi kuwa haikuwa kazi rahisi sana kukubaliana na wazo la Richie, lakini kwa jitihada kubwa kutoka kwa Richie pamoja na watu wake wa karibu akiwemo mama yake mzazi, hatimaye alijikuta akikubali kujiunga na kundi la maigizo la Nyota Assemble.
“Kila nilipokuwa nikikataa, Richie alizidisha ushawishi, lakini pia hata ndugu zangu wa karibu akiwemo mama waliendelea kunisisitiza kuwa nafaa kabisa kuigiza na kwamba ndiyo karama na kipaji ambacho wanaamini Mungu alinizawadia kulingana na wao walivyokuwa wakiniona,” anasema.
JB anasema, licha ya kukubaliana na wazo la Richie, lakini hakujiunga moja kwa moja, akawa anawaahidi lakini siku ikifika, anaingiza visingizio vingi, hali iliyomlazimu mama yake mzazi kuingilia kati kwa kumuonya na udanganyifu aliokuwa akiwapa wenzake (akina Richie) kwa kuwaahidi jambo ambalo ilikuwa ni ngumu kulitekeleza.
“Mama ikabidi akomae na mimi bwana, kusema ukweli nilikuwa nimekubali kwa maana ya kuwaridhisha tu lakini sikuwa nimeafiki kwa kumaanisha kabisa, akili na mawazo yangu yote yalikuwa kwenye biashara tu na si kitu kingine,” anasema JB.
Wakati mazungumzo yanaendelea, ghafla ninamuona JB akinyamaza kimya kidogo huku shingo yake akiwa ameielekeza mahali kwa muda mrefu, nikalazimika kugeuka na kutazama mahali alipokuwa amegeukia.
Lilikuwa ni kundi la watoto wa mitaani wakipita huku na kule wakitafuta riziki, kufika hapo nikamuona JB akiinuka na kuwapungia mikono kwa ishara ya kuwaita, bila kuchelewa walikuja haraka sana hadi mahali tulipokuwa tumekaa na kumkumbatia JB bila uoga wowote huku naye akionekana kuwafurahia.
JB alitumia muda mwingi sana kuzungumza na watoto hao akiwatia moyo kuwa maisha ya tabu waliyokuwa wakiishi ni ya muda tu kwamba wasijisikie vibaya huku akiwataka waendelee kuwa na tabia njema kwa watu na kumheshimu kila mtu aliyeko mbele yao, ambapo kwa pamoja watoto hao waliitikia kwa furaha.
Hapohapo nikamuona JB akilala ubavu kidogo kisha kuchomoa waleti yake ya gharama na kuifungua na kutoa noti nyingi sana nyekundu, akawapa wale watoto waliokuwa zaidi ya 7, kila mmoja shilingi 10,000 na kuwataka watupishe kwa ajili ya mazungumzo yetu.
“Unajua ipo siri ambayo watu wengi sana hawaijui, ni siri ya kutoa na kusaidia wengine, ili Mungu akubariki, ni lazima uwe na moyo wa kutoa, kusaidia watu kwa kadiri unavyoweza, Mungu hawezi kukuacha kama ulivyo, amini maneno yangu mdogo wangu (mwandishi),” anasema JB huku akifungua chupa yake ya maji na kunywa taratibu.
“Basi bwana ngoja tuendelee, siku moja nikaona ngoja nikawatembelee kwenye ukumbi wao wa mazoezi, nilipofika nikaanza kwa kuchungulia kwanza kabla sijaingia ndani kabisa, nilichokishuhudia humo sikutaka hata kugeuka nyuma, haraka nikaondoka huku nikijiapiza kutorudia tena, na hata mpango wa kujiunga na uigizaji nikautoa kabisa akilini mwangu,” anasema JB.
Je, JB ameona nini? Usikose kufuatillia wiki ijayo.