Gladness Mallya
MSICHANA Ramla Mohamed (31) mkazi wa Tandika, Dar amejikuta katika wakati mgumu kutokana na kufungiwa ndani kwa miaka 25 baada ya kupooza uti wa mgongo na kusumbuliwa na degedege.
Tukio hilo liligundulika hivi karibuni baada ya majirani kutoa taarifa kwenye serikali ya mtaa kwani mama wa msichana huyo, Moza Athuman kwa miaka yote 25 alikuwa akimfungia ndani na kwenda kwenye shughuli zake na hakuwahi kumtoa nje hata siku moja.
Akiwa na mama yake.
“Ukweli inauma sana kwani huyo msichana hatujawahi kumuona akitolewa nje hata siku moja, mama yake huwa anamfungia tu ndani kila kitu ni hukohuko, haja kubwa na ndogo ni hukohuko ndani mama yake anatoa nje kwenye chombo chake maalum, sisi tukaona bora tuwaambie watu wa serikali wanaweza kumsaidia.
“Alianza kuugua akiwa na miaka mitano hivi ila cha kushangaza wajumbe waliofika nyumbani kwa mgonjwa huyo walianguka na kupandisha mapepo,” alisema jirani mmoja ambaye hakutaka jina lake lichorwe gazetini.
Alipoulizwa mama wa msichana huyo sababu za kumfungia mwanaye, alisema kwamba kutokana na mumewe kumtelekezea mtoto huyo hana msaada wowote wa kumtoa nje na kumrudisha ndani pia kumpeleka kwenye mazoezi hospitali.
“Mwanangu alizaliwa akiwa mzima lakini alipofikisha miaka mitano akaanza kuugua, nikampeleka hospitali akagundulika kuwa ana ugonjwa wa degedege na amepooza uti wa mgongo hivyo nikaambiwa anahitaji kupelekwa mazoezi kila wiki, kutokana na ugumu wa maisha nikashindwa ndiyo maana namfungia ndani tu,” alisema mama huyo.
Naye mwenyekiti wa mtaa huo wa Azimio, Mwishehe Issa alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na wajumbe wake kudondoka ambapo alisema kwa kupitia vyombo vya habari kwa yeyote akayeguswa ajitokeze kumsaidia msichana huyo.