MAKUNDI yanayomuunga mkono Waziri Mkuu Edward Lowassa yametangaza kutokiunga mkono Chama cha Mapinduzi na kuhamishia kampeni zake kwa mgombea urais atakayesimamsihwa na vyama vinavyounda kundi la Umoja wa Katiba ya wananchi (Ukawa).
Wakizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es salaam, viongozi wa makundi hayo ambayo ni pamoja na Four U Movement, Lowassa for Presidency, Shirikisho la Walimu, Madereva wa bodaboda na Temeke Jogging na Youth Movement walisema wamekasirishwa na ukiukwaji wa kanuni katika vikao vya CCM.
Akizungumzia hatua hiyo, kiongozi wa Four U, Hemed Ali alisema kwa kuwa wameshindwa kupata mabadiliko ndani ya CCM wanakwenda kuyatafuta Ukawa.
“Tunatangaza rasmi kama vijana tuliokuwa tunamuunga mkono Lowassa, sasa tunaunga mkono Umoja wa Katiba ya Wananchi yaani Ukawa,” alisema Hemed.
Wakati mkutano huo ukiendelea vijana wa makundi hayo walikuwa wakishangilia na kuonyesha nembo za Chadema.
Mapema wiki hii vinaja wengine zaidi ya 40 wa kundi la Four U movement, walirudisha kadi za CCM na kuchukua kadi za Chadema katika ofisi za wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.