Thursday, July 16, 2015

MFAHAMU Mwanafunzi Aliyeongoza Matokeo ya Kidato Cha Sita TZ

Wakati Ramadhani Gembe anafanya
mtihani wa Taifa wa kidato cha sita miezi
miwili iliyopita, hakuwahi kufikiri
angeshika namba moja kwa ufaulu kitaifa
licha ya jitihada zake za kujituma.
Lakini siku zote Mungu hamtupi mja
wake. Kama jina lake linavyosadifu
mwezi mtukufu unaomalizika siku mbili
zijazo, Ramadhani ambaye amehitimu
Shule ya Wavulana ya Feza jijini Dar es
Salaam, ameibuka mwanafunzi bora
nchini kati ya waliofanya mtihani huo wa
kujiandaa kwa masomo ya elimu ya juu.
“Nilitegemea ningefaulu lakini siyo kwa
kiwango hicho… hii ni
‘surprise’ (shtukizo),” alisema Gembe
alipohojiwa na Mwananchi baada ya
matokeo ya kidato cha sita kutangazwa
na Baraza la Mitihani la Taifa.
“Nawashukuru wazazi, walimu, ndugu na
wanafunzi wenzangu kwa kunipa
ushirikiano. Nilikuwa nafanya sana ibada
hivyo haya matokeo ni juhudi binafsi na
majibu ya Mungu,” alisema Ramadhani
aliyesoma mchepuo wa fizikia, kemia na
baiolojia (PCB).
Historia ya Ramadhani darasani si haba
kwani mwaka 2008 alikuwa ni
mwanafunzi pekee aliyejiunga na shule
ya vipaji maalumu ya Ilboru, Arusha
akitokea shule ya Msingi Mombo na
alipata daraja la kwanza akiwa na pointi
11 katika matokeo ya kidato cha nne.
“Siku zote kilichonifanya niongeze juhudi
katika masomo yangu ni malengo ya
baadaye… mimi nataka kuwa daktari wa
binadamu hivyo sikutaka kulegalega
kusoma. Pia, wazazi wangu pamoja na
hali ngumu walijitahidi kunisaidia
kimawazo, kirasilimali na kimaadili…
naomba na wazazi wengine wawafanyie
hivyo watoto wao,” alisema.
Nurdin Gembe, ambaye ni mzazi wa
Ramadhani, alisema familia imepokea
kwa furaha matokeo hayo na kwamba
alikuwa akiyategemea kuwa mazuri
kutokana historia ya kijana wake katika
madarasa ya nyuma.
“Huyu mtoto namlea kawaida japo
zamani alikuwa mtundu sana… ilibidi
nimpe mafundisho mengi sana ya kidini
bila kupoteza ratiba ya kusoma shuleni.
Nashukuru kuwa alizingatia na amefika
hapo alipofika,” alieleza Gembe ambaye
ni bwana shamba kitaaluma.
Kwa upande wake Yonazi Senkondo,
aliyeshika nafasi ya tisa kitaifa, alisema
matokeo hayo ni majibu ya maombi kwa
Mungu na juhudi zake kusoma na
ushirika na wanafunzi wenzie.
“Siku zote nilikuwa naombea niingie 10
bora, najua leo Mungu amejibu maombi
yangu. Nilikuwa nafanya mijadala na
wanafunzi wenzangu hasa huyo
aliyeshika namba moja. Sishangai yeye
kuwa katika ngazi hiyo.