Wednesday, July 8, 2015

MTANGAZAJI MAARUFU, 'GODWIN GONDWE' AMWAGA MACHOZI HADHARANI, SOMA HAPA KILICHOMSIBU

MTANGAZAJI maarufu ambaye pia ni Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Mlimani, Dar na
Mshereheshaji (MC), Godwin Gondwe ‘Double
G’ wikiendi iliyopita alimwaga machozi
hadharani wakati akitoa ushuhuda wa maisha
aliyopitia wakati wa semina ya ujasiriamali
inayofanyika kila Jumapili katika Ukumbi wa
Kituo cha Mafuta cha Victoria, kilichopo
Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
Katika tukio hilo ambalo huratibiwa na kikundi
cha Kusifu na Kuabudu cha Glorious Worship
Team (GWT), Gondwe alisema anashangazwa
na hatua aliyofikia katika maisha yake, kwani
aliishi kwa taabu na kufanya kazi ambazo
wakati mwingine zilihatarisha afya yake, lakini
kwa uwezo wa Mungu, amevuka na sasa
anamshukuru.
Akiwa katika hisia kali, Gondwe alitokwa na
machozi wakati akikumbuka maisha aliyopitia
na kuwaambia mamia ya watu waliohudhuria
semina hiyo kuwa anahisi uwepo wa Mungu
ndani yake na kwamba machozi anayotoa ni
mapokeo na sifa kwa Muumba juu ya yote
aliyomtendea hadi sasa.
“Nimetoka kwenye familia ya kawaida sana,
maisha yangu yamejaa mihangaiko na
shuhuda nyingi ngumu, lakini kubwa ni
kufanya kazi ya kutunza choo katika hospitali
ya wagonjwa wa kifua, tena bila mipira
(gloves), jambo lililohatarisha sana afya
yangu,” alisema mtangazaji huyo na kuongeza;
“Pia, niliwahi kuwa mhudumu wa hoteli, yote
hayo ni kule Mwanza, kwa hiyo kufika hapa ni
kwa neema ya Mungu tu, nawaomba watu
wasikate tamaa, wasikubaliane na hukumu ya
binadamu na wala mazingira yasiwaamulie
hatima yao, waseme I’m what God says I’m
(Niko hivi nilivyo kutokana na jinsi Mungu
anavyotaka).
“Pia, tusisahau kumshukuru Mungu kwa
kumtolea, maana anasema nijaribuni kwa
matoleo, yaani leo hii niko hapa! Hakika huyu
ni Mungu, kila kitu kinawezekana,” alisema
Gondwe na kuwataka watu kutomsahau Mungu
kwa kumtolea kwa kila mafanikio wanayofikia,
kwani ndiyo siri kubwa ya maisha.
Mbali na mtangazaji huyo, pia mwalimu mahiri
nchini wa kuhamasisha watu kujikomboa na
umaskini, Eric Shigongo alitoa somo la jinsi
ambavyo mke, mume au mchumba
wanavyoathiri maisha yetu, somo ambalo
litaendelea wiki hii.
Tamasha la GWT Sunday Celebration,
hufanyika kila Jumapili katika ukumbi huo bila
kiingilio ambapo watu hufundishwa mbinu
mbalimbali za kujikwamua na umaskini kutoka
kwa walimu mahiri pamoja na kusifu kwa
kuabudu.