Sunday, August 16, 2015

Diamond akubali Mil. za Ukawa kwa ajili ya kumfanyia kampeni Lowassa!


Staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ amekubali kuwa yupo tayari kupokea mamilioni ya fedha kwa ajili ya kumfanyia kampeni mgombea urais kupitia muunganiko wa vyama vya upinzani Bongo vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Ngoyai Lowassa.

LICHA YA URAFIKI NA JK

Habari za uhakika kutoka chanzo cha kuaminika ambacho ni mtu wa karibu wa Diamond zilidai kwamba, licha ya jamaa huyo kuwa na urafiki na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete ‘JK’ ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), lakini mbele ya mkwanja anaweza kuamua tofauti.



LOWASSA VS MAGUFULI

Chanzo hicho kilieleza kwamba, jamaa huyo amekuwa akishawishiwa kujipambanua kuwa atamfanyia nani kampeni kati ya Lowassa na Dk. John Pombe Magufuli wa CCM zitakazoanza Agosti 22, mwaka huu.

“Unajua hata kipindi kile wakati Lowassa anatangaza nia Arusha, jamaa (Diamond) alikwenda kwenye shoo kwa sababu ya mkwanja tu lakini ukweli ni kwamba alikuwa upande wa Bernard Membe (naye alikuwa mtia nia wa CCM).

KWENYE MTONYO

“Unajua Dangote (Diamond) linapokuja suala la mtonyo, huwa halazi damu. Ukweli anaomba Mungu tu mamilioni yatue mikononi mwake maana yeye siyo mwanasiasa ni mfanyabishara kupitia muziki.

“Anakwambia muziki ni biashara kama biashara nyingine. Ni kama kuuza maji, haijalishi wewe ni chama gani lazima utahitaji maji au huduma nyingine yoyote bila kujali siasa,” kilidai chanzo hicho kwa sharti la kutotajwa gazetini na kuongeza:

“Huo ndiyo msimamamo wa wasanii wengi, Ukawa wakileta mzigo watapatiwa huduma yao na CCM nao wakija watapewa huduma wanayohitaji. Ni kama siti ya daladala, haijalishi anayekalia ni Chadema au CCM.”

KUTOKA NDANI YA UKAWA

Duru za kisiasa kutoka ndani ya Ukawa zilidai kwamba, tayari fungu limetengwa kwa ajili ya wasanii watakaozunguka na mheshimiwa (Lowassa) Tanzania nzima kwa ajili ya kampeni.

“Diamond ni mmojawapo lakini wasanii watakaokuwa bega kwa bega na Lowassa ni wengi. Kuhusu kama wameshasaini mikataba hilo lipo wazi kwani time (muda) yoyote watadakishwa mamilioni yao,” kilisema chanzo chetu ambacho ni mmoja wa wasanii walio ndani ya Team Lowassa tangu akiwa CCM.

DIAMOND AFUNGUKA

Baada ya kunyetishiwa habari hizo, gazeti hili lilimtafuta Diamond ili kujua kama ameshakabidhiwa mamilioni hayo na kwamba anayazungumziaje?

Ijumaa: Mambo vipi Baba Tiffah?

Diamond: Poapoa. Inakuwaje?

Ijumaa: Princess Tiffah na mama’ke hawajambo?

Diamond: Wako poa sana, namshukuru Mungu, hapa nipo jikoni nawaandalia madikodiko, si unajua tena?

Ijumaa: Oke. Kwanza hongera kwa sababu kuna habari imetufikia kwenye Dawati la Ijumaa kwamba, umevuta mamilioni ya Ukawa. Hii ishu ikoje?

Diamond: Habari njema hizo. Sijasaini mkataba lakini nazingoja kwa shauku kubwa.

Ijumaa: Nasikia wanakutafuta sana hao Ukawa, je, umeshaongea nao?

Diamond: Mimi ni mwanamuziki wa Tanzania, nina haki ya kwenda kumburudisha Mtanzania yeyote ikiwa ametimiza hitaji la malipo yanayotakiwa kwa shughuli yake.

Haitakiwi Ukawa wala CCM kunilaumu kwa namana yoyote ninapokwenda kutoa huduma ya burudani.

Mimi napokea simu nyingi za biashara na mimi ni mfanyabishara, kwa nini dili likija nisilichukue? Dili lije nalisubiria.