Thursday, August 20, 2015

Hivi ndivyo Waziri alivyozua timbwili

Waziri Kamani balaaWaziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Dk. Titus Kamani na maofisa polisi.
KUFUATIA tukio la Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Dk. Titus Kamani juzikati kugeuka ‘bondia’ kwa ‘kumwanzishia’ timbwili msimamizi wa uchaguzi wa marudio wa kura za maoni ya ubunge kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Busega, Simiyu na kusababisha matokeo yasitangazwe, wadau wameibuka na kusema yote hayo ni machungu ya kukatwa.
Katika tafrani hiyo, miwani ya Waziri Kamani ilivunjika akiwa katika harakati za kumkabili msimamizi huyo ambaye ni Katibu wa CCM Wilaya ya Meatu, Jonathan Mabihya wakati akitangaza matokeo.
Vurugu hizo zilizozuka majira ya saa 4:18 asubuhi ambapo askari polisi waliwatia mbaroni watu kadhaa, zilisababisha Mabihya kushindwa kutangaza matokeo na kuahirisha kwa muda huku Mkuu wa Wilaya ya Busega, Paul Mzindakaya akisema yatatangazwa baada ya utulivu kurejea.
Baada ya tukio hilo, Waziri Kamani akiwa amefura kwa hasira, alielekea kwenye gari lake lenye namba za usajili T 196 AMD lililoegeshwa nje ya ofisi ya CCM ambapo wapambe wake walimsogelea na kumtuliza.
Baadhi ya wanachama wa chama hicho walipoongea na Amani walisema uchaguzi wa mwaka huu umekuwa tofauti na miaka mingine kwani wagombea wamekuwa wakipandwa na hasira pale majina yao yanapokatwa huku wengine wakitangaza hata kuhama chama.
“Waziri Kamani hakuwa na tatizo jingine. Alishajua jina lake limekatwa (ameanguka kwenye kura). Kwa hiyo zile vurugu ni hasira. Unajua alikuwa anapigana kutetea nafasi yake ya uwaziri. Kwa hiyo kitendo cha kukatwa maana yake nini? Uwaziri wake upo shakani,” alisema mwanachama mmoja.
Naye mkuu wa wilaya, Mzindakaya alipozungumzia vurugu hizo, alisema:  “Mshindi ameshapatikana, kitendo alichofanya Waziri Kamani kinamshushia hadhi.”
Akizungumza na wana habari kabla ya kuondoka eneo la tukio, Waziri Kamani alisema matokeo ya uchaguzi huo hayajatangazwa, yameandaliwa katika mazingira ya hujuma na kuwatuhumu wasimamizi na Dk. Raphael Chegeni ambaye ndiye alikuwa mpinzani wake mkuu.
“Hii ni hujuma dhidi yangu. Hili limefanywa makusudi. Watu wamekesha ndani, usiku kucha wakinywa pombe, wakiandaa matokeo bila kuwepo mawalaka wetu. Wagombea tumeomba tuhakiki wakakataa,” alisema Waziri Kamani.
Hata hivyo, Agosti 17, mwaka huu, Kamati Kuu ya CCM (CC) iliyokaa jijini Dar chini ya mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete ilimpitisha Dk. Chegeni kuwa mshindi wa kinyang’anyiro hicho ambapo kwa kura za maoni alipata 13,859 dhidi ya 11,553 alizopata Waziri Kamani. Ni kati ya kura 26,277 zilizopigwa ambapo kura 430 ziliharibika.