Mashaka Kisusi
NJEMBA wawili ambao ilisemekana ni wapiga debe, wamejikuta wakizichapa kavukavu wakigombea mzigo wa abiria.
Tukio hilo lililojaza watu ambao walikuwa wakishangilia wakati njemba hao ambao majina yao hayakuweza kupatikana mara moja wakizichapa, lilitokea hivi karibuni majira ya saa 6 mchana ndani ya kituo cha Mabasi cha Nyegezi, jijini Mwanza.
Kwa mujibu wa mashuhuda, jamaa hao walitofautiana baada ya abiria mmoja kushushwa na daladala ambapo walianza kugombea mzigo wake.
“Walikuwa wakigombea mzigo wa abiria sasa huyu mwenye T-Shirt ya njano alionekana kumzidi nguvu mwenye T-Shirt nyeusi, kuona hivyo, mwenye T-Shirt nyeusi alimtwisha mwenzake kichwa cha uso hadi kumtoa nundu,” alisema shuhuda huyo na kuongeza:
“Baada ya jamaa (mwenye T-Shirt nyeusi) ku-’wini’ kihivyo, alimchukua abiria na mzigo wake wakaondoka na kumuacha mwenzake (mwenye T-Shirt ya njano) akijichua nundu yake.
“Nundu ilikua kwa kasi kiasi cha kuwafanya wapiga debe wenzake waanze kumcheka ambapo alipatwa hasira sana akaanza kumsaka mwenzake ili alipize kisasi,” alisema shuhuda.
Hata hivyo, mashuhuda wakiwemo wapiga debe wenzao, waliingilia kati kwa kumchukua mwenye T-Shirt nyeusi kumpeleka eneo jingine na kumuacha mwenye T-Shirt ya njano akimtangazia mwenzake kuwa hiyo vita haijaishia hapo, itaendelea siku nyingine!