Treni ya abiria kuanza safari zake hivi karibuni
Miezi kadhaa baada treni ya kubeba abiria jijini Dar es Salaam kusitisha safari zake kutokana na ubovu, imeelezwa kuwa hali hiyo ni kutokana na uchakavu wa injini.
Mkuu wa Masoko wa Kampuni ya Reli Tanzania, Charles Ndenge alisema treni hiyo imekuwa ikiharibika mara kwa mara, kutokana na injini zake kutumika kwa muda mrefu, huku treni hiyo ikifanya kazi tofauti na ilivyoundwa.
“Treni hii ilitengenezwa kwa safari za mbali, hata hivyo imeshafanya kazi kwa muda mrefu na injini zake zimechoka ndiyo maana zinafanyiwa marekebisho niwahakikishie watumiaji huduma ya usafiri itarejea kama kawaida” alisema Ndenge.
Alifafanua mpaka sasa matengenezo yamefika katika hatua nzuri na wiki mbili zijazo huduma hiyo itaanza kufanya kazi tena.
Ili kuepukana na adha ya kusitishwa kwa huduma hiyo mara kwa mara, Ndenga alisema kwamba kunahitajika treni iliyotengenezwa maalumu kwa ajili ya safari za mjini.
“Usafiri wa treni kwa safari fupi unaweza kuwa imara endapo kutakuwa na treni zilizotengenezwa maalumu kwa ajili ya kazi hiyo mikakati ambayo inaendelea, lakini hatuwezi kuizungumzia kwa sasa”alisema.
Aliweka wazi kwamba matengenezo ya injini hizo yanaendelea na wiki mbili zijazo huduma hiyo ya usafiri inaweza kurejea.
Kusitishwa kwa huduma hiyo ya usafiri kumeleta kero kubwa kwa wakazi wa Dar es Salaam, ambao wamekuwa wakitegemea njia kukabiliana na changamoto ya foleni hasa nyakati za asubuhi na jioni.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, baadhi wa watumiaji wa usafiri huo walidai kuwa kukosekana kwa treni kumesababisha kuathirika kwa shughuli zao za kiuchumi kutokana na kutumia muda mwingi kwenye foleni.
“Treni ilikuwa inasaidia sana, lakini sasa hivi tunalazimika kupoteza muda mwingi kwenye foleni za daladala, hivyo tunaomba wahusika waliangalie suala hili kwa umakini zaidi usafiri wetu walala hoi urejee”alisema Erick Kivambala mkazi wa Ubungo Jasmine Ally mkazi wa Tabata alisema kukosekana kwa usafiri huo, kumeleta changamoto kubwa kwa wanafunzi ambao wamekuwa wakipata wakati mgumu kwenye daladaa kutokana na kusumbuliwa makondakta.
“Ingawa hata watu wazima tumeathirika lakini wanafunzi ndiyo wameathirika zaidi, maana treni ndiyo ilikuwa inawabeba bila matatizo yoyote, siku hizi unawakuta kwenye vituo vya daladala wakikunjana mashati na makondakta”alisema.
Kwa upande wake Ofisa Habari Mkuu Wizara ya Uchukuzi, William Budoya Ndenge alikiri kuwepo kwa kadhia hiyo na kueleza kuwa treni maalum kwa ajili ya safari za mjini zinahitajika kukabiliana na changamoto za usafiri katika maeneo hayo.
“Ili usafiri huu uwe wa uhakika ni lazima ziwepo treni ambazo zimetengenezwa maalum kwa ajili ya kutoa huduma za usafiri maeneo ya mijini,”alisema.
Kuhusiana na madai ya kuwepo kwa mvutano kati ya TRL na Wizara ya Uchukuzi katika suala la uendeshaji wa treni hiyo, Budoya alisema jambo hilo halina ukweli na wamekuwa wakishirikiana bega kwa bega kuhakikisha huduma hiyo inarejea.
“Sisi tunatunga sera na TRL ni waendeshaji tunatambua fika kwamba treni hili ni mkombozi kwa wakazi wengi wa Dar es Salaam, ndiyo maana tunaweka nguvu zote kuhakikisha linarejea”alisema Budoya