Majeneza ya wanafamilia watatu, Elimringi Minja, 60 (baba), Tudetsiwe Sanga, 48 (mke) na mtoto wao, Haikaeli John (10).
Stori: Na mwandishi wetu
BADO ni kilio! Bado ni simanzi katika Kijiji cha Marangu, Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro kufuatia vifo vya wanafamilia watatu, Elimringi Minja, 60 (baba), Tudetsiwe Sanga, 48 (mke) na mtoto wao, Haikaeli John (10).
…Ndugu, jamaa na marafiki wakielekea mazikoni kwa ajili kusitili miili ya marehemu hao.
Watatu hao maisha yao yalikatishwa kwenye ajali ya Basi la Metro iliyotokea Septemba 15, mwaka huu katika eneo la Manga, Handeni mkoani Tanga na hivyo kuiacha nyumba yao katika ukimya wa maisha bila wao hata kama wataishi watu wengine.
Kufuatia vifo hivyo, baadhi ya watu kijijini hapo walizungumzia maisha ya marehemu hao ya siku mbili kabla, hususan mke na mume huku wakionesha imani yao kwamba, kufa kwa watu hao kuna mkono wa mtu.
“Kama kweli binadamu tungepewa kuona kiroho, mzee Elimringi asingekufa. Siku mbili kabla ya tukio nilikutana naye, akasema alichofuata Dar kimekamilika, lakini anafikiria kusafiri Jumatano kurudi Moshi (Septemba 16) badala ya Septemba 15 siku ya Jumanne.
“Nilimuuliza kwa nini asiondoke Jumanne, akasema anaiona kama siyo siku ya safari. Lakini jioni yake akaniambia aliamua kusafiri Jumanne na familia yake na alishakata tiketi.
“Alisema kama kuna lolote baya acha litokee. Kumbe kweli baya lilikuwepo mbele yake. Ina maana aliliona kwenye ulimwengu wa kiroho. Binadamu tunatakiwa kusali sana, roho wa mauti anatuzunguka usiku na mchana. Lakini mimi naona kama kuna mkono wa mtu uliowamaliza wanafamilia hao. Ingawa maisha ya marehemu na familia yake hawakuwa na matatizo na watu,” alisema mzee Paschal, mkazi wa Dar aliyeshiriki mazishi hayo.
Mwanamke mmoja aliyejitambulisha kwa jina la mama Jane akimzungumzia marehemu, Tudetsiwe alisema:
“Nalia mwanangu. Hapa si bure! Nalia bado kwa ajili ya kifo cha mama Haikaeli. Kinaniuma sana. mama Haikaeli mara ya mwisho nazungumza naye tulicheka sana, akasema tucheke kwa sababu kifo kipo na tukifa hatutaweza kucheka tena. Leo hii kweli yeye hawezi kucheka tena! Inauma sana.”
Majeruhi mmoja aliyelazwa Kituo cha Afya cha Mkata, Tanga alisema:
“Namshangaa sana Mungu mimi kuwa hai. Sina jema lolote lililomshawishi kunibakiza. Lakini ndani ya basi lile siku ile roho ya mauti ilitawala kwani tangu Dar abiria hatukuwa na mazungumzo mengi kama inavyokuaga ndani ya mabasi. Ukimya ulitawala. Ningejua nisingepanda lile basi.”
Marehemu Elimringi ambaye alikuwa Mwalimu Mkuu Shule ya Mbahe, Moshi Vijijini na familia yake walizikwa Septemba 18, mwaka huu kwenye kijiji hicho huku wachungaji na mapadri walishiriki kwenye ibada ya mazishi.