Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema kupitia mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa amesema kuwa ataunda tume ya maridhiano itakayoshughulika migogoro ya wakulima na wafugaji ili kuondokana na matatizo ambayo yamekuwa yakiwasumbua.
Lowassa amesema tume hiyo ndiyo itakayokuwa mwarobaini wa matatizo ya wakulima na wafugaji nchini ambao wamekuwa wakipigana na kuleteana matatizo ambayo yamechukua muda kutatuliwa.
Mgombea huyo amesema hayo yatawezekana pale tu atakapochaguliwa kuingia madarakani katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Akizungumza jana na wananchi wa Matui ambao wengi wao ni wakulima na wafugaji katika uwanja wa Soweto wilayani Kiteto Lowassa alisema tume hiyo itapitia matatizo yote ya wakulima na wafugaji na kutoa suluhisho la uhakika.
“Serikali yangu itapitia migogoro hiyo na kulipa fidia zinazostahili kwa wale walioathirika na migogoro iliyoibua mapigano kati ya wakulima na wafugaji katika maeneo mbalimbali nchini,”alisema Lowassa huku akishangiliwa na wananchi hao.
Alisema wakishalipa fidia hizo na kutatua migogoro hiyo matatizo kati ya wakulima na wafugaji hayatajirudia tena.
Katika Wilaya ya Kiteto kumekuwa na mgogoro wa wakulima na wafugaji ambao umekuwa ukizungumzwa katika Bunge la 10 ukihusishwa pia na wakazi wa Wilaya ya Kongwa.
Lowassa alisema kuwa serikali yake itapima ardhi yote nchini ili kutambua maeneo ya wakulima na wafugaji ili wasiweze kuingiliana na kuleteana shida.
Kwa upande wake aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ole Medeye alisema Lowassa akiingia madarakani matatizo ya wakulima na wafugaji yatatatuliwa ndani ya miezi miwili nchini kote.
Ole Medeye alisema kuwa Waziri Mkuu ameshindwa kutatua migogoro ya ardhi nchini na badala yake amekuwa akitalii tu katika maeneo hayo badala ya kusikiliza matatizo ya wananchi.