Monday, September 14, 2015

MCHAMBUZI WA KIMATAIFA ATUPA SWALI KWA WAGOMBEA URAIS TANZANIA,..JE TUNATOA AHADI ZINAZOPIMIKA AU ORODHA YA MATUMAINI? - 2


Na Mwandishi Wetu, Addis Ababa
WIKI iliyopita niliendelea kufanya uchambuzi kuhusu maudhui na muktadha wa Ilani za Uchaguzi za kambi mbili zenye ushawishi katika siasa za mwaka huu; CCM na Ukawa.  Tulianza kutumia vigezo vitatu kupima ahazi za kila Ilani zinaweza kupimika utekeleza wake au ni ahadi tu za matumaini!
Vigezo nilivyotumia ni kama kuitazama ahadi yenyewe iwapo inakidhi hoja ya kuwa suala linalohitaji kuwekwa katika ilani?Pili tukifungua boksi tutaona ni mkakati gani ilani inauainisha wa kutekeleza kilichoahidiwa na Je, ilani inaweka kigezo kinachopimika kwa maana miaka mitano baadaye tukupime vipi kwa lengo lipi?
Tulizichambua sekta za elimu na maji katika kuangalia Ilani zimeahidi masuala yanayoweza kupimika? Tulibainisha changamoto katika Ilani hasa ya Ukawa kukosa kuwa na mkakati wa utekelezaji lakini na vigezo vinavyopimika.
Kwa mfano, tuliona, katika sekta ya maji Ilani ya Ukawa iliahidi tu: “Tutaweka mazingira rafiki yatakayomhakikishia kwa kila Mtanzania kupata maji safi na salama. Kumaliza kero za maji nchini kutamkomboa mwanamke kutokana na adha ya kuchota maji kwa kichwa.”
Tamko hilo la “mazingira rafiki” halikufafanua sit u mazingira rafiki ni yapi, lakini lengo ni kuwafikishia maji watanzania wangapi kufikia mwaka 2020 au kuchimba visima vingapi au kukarabati mabomba au mifumo mingapi.

Hiyo ilikuwa tofauti kabisa na Ilani ya CCM ambayo kiuchambuzi imetimiza vijenzi vyetu vitatu vya hoja hapo juu. Kwa mfano inasema: “Kuboresha huduma ya maji vijijini kutoka asilimia 53.4 mwaka 2015 hadi asilimia 70 mwaka 2020 kwa kufanya yafuatayo….”

Tulijenga hojan kuwa ilani hizi mbili katika eneo hili ni milima miwili tofauti kabisa. Ukawa wanamaanisha kuwa hawana mikakati ya utekelezaji wa wanachoahidi na watasubiri kuingia Ikulu ndio waanze kuangalia cha kufanya. Unaposema tu “tutaweka mazingira rafiki ya kila Mtanzania kupata maji safi na salama” kunaibua maswali.
Mosi ni mazingira gani hayo “rafiki?” Pili yatawekwa lini na mwisho unaposema “kila Mtanzania” tunamaanisha nini. Kwamba kufikia mwaka 2020 kila Mtanzania atakuwa na maji safi na salama?
Leo tunaendelea kwa kufanya ulinganisho na uchambuzi kama huo kwa kuangalia Ilani hizo katika sekta za kilimo, nishati na sera za mambo ya nje.

  Kilimo
Kilimo ni sekta nyeti sana nchini. Takwimu bado zinaonesha asilimia zaidi ya 70 ya Watanzania wanategemea kilimo. Hii haishangazi kuona Ilani zote mbili; CCM na Ukawa zikiwa na mambo mawili matatu maboresho katika sekta hii.
Ukawa wanazungumza mambo manne makubwa kuhusu kilimo. Mosi ni kuhakikisha sekta hiyo inakua kwa asilimia 6-8. Pili, umwagiluiaji. Tatu, maghala ya kuhifadhi mazao na nne kilimo cha biashara.
Lakini tatizo langu ni lile lile, ukiacha walivyojitutumua katika ahadi ya kwanza hapo juu kwa kuonesha namna tutakavyowapima miaka mitano ijayo (ahadi inayopimika ya kukuza kilimo kwa asilimia 6-8) ahadi zilizobaki ni matamko tu hauonekani mkakati wala kigezo cha kuwapima.
Hii ni tofauti na CCM ambao katika ahadi zao za kipaumbele katika sekta ya kilimo kila moja imewekewa malengo tutakaowapima nao. Mfano, ili kuendelea kuwafikia wananchi wengi na kuwapa elimu ya kilimo imewekwa lengo la kuajiri maafisa ugani kufikia 15,082 kutoka 9,558 wa sasa.
Kuhusu kilimo cha umwagiliaji ilani imefanya uchambuzi na kubaini pamoja na wakulima wengi kwa sasa kuanza kuhamia katika umwagiliaji badala ya kutegemea mvua pekee bado lengo ni kuongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka ekari 461,362 za sasa hadi ekari 1,000,000 mwaka 2020 na ukurasa wa 12 wameainisha wataitekeleza vipi ahadi hii.
Hii inampa mwananchi si tu Imani bali uhakika wa kufuatilia ahadi na kuona utekelezaji wake. Ilani ya Ukawa hapa tena haikuwatendea haki wananchi inaoahidi kuwaletea mabadiliko.
Nishati
Sekta ya nishati ni sekta nyingine muhimu kijamii na kiuchumi na imetendewa haki katika ilani zote mbili. Ukawa na CCM wote wameweka lengo wanalotaka tuwapime nalo miaka mitano ijayo la kuongeza/kuzalisha megawati 3,000 (Ukawa) na 4,915 (CCM).
Vyama vyote vimetaja vyanzo mbalimbali vya uzalishaji wa umeme watakavyovitumia kama vile gesi asilia, maji na vyanzo vingine mbadala. Tatizo langu na ndio moyo wa makala hizi ni Je, tunatekeleza vipi ahadi hizi tamu tunazoahidi?
Katika ilani ya “mabadiliko” ya Ukawa hakuna vijenzi vya hoja yao hiyo. Hakuna ainisho la mitambo watakayoijenga ya kuzalisha na kusambaza umeme itakuwa wapi na kila mmoja utazalisha megawati ngapi. Kwa ujumla ilani imemwaga tu ahadi, labda wakishaingia Ikulu ndio watazinduka!
CCM wamekuwa “smart” katika hili na kama ilivyo katika maeneo mengi. Kwanza wameanisha watakavyozizalisha hizo megawati walizoahidi na wanavyoboresha mfumo wa usambazaji.
Katika uzalishaji Ilani inaahidi kutekeleza miradi ya umeme iliyoainishwa katika Mpango Kabambe wa Uzalishaji wa Umeme ambapo kwa ufahamu wangu imo mitambo ya uzalishaji wa umeme wa gesi minnee Dar es Salaam (ikiwemo Kinyerezi 1 ambayo iko tayari) na mingine Mtwara na mingine ya vyanzi anuai. Hawa wanamkakati tayari.
Kuhusu mifumo mipya ya kusambaza umeme (maana unaweza ukawa na umeme na usiwafikie wananchi), CCM wametaja kukamilisha miradi mikubwa ya ujenzi wa mifumo mipya ya usambazaji kama vile Mradi waBackbone wa kV 400 unaounganisha mikoa ya Iringa, Dodoma, Singida na Shinyanga wenye urefu wa km 670;

Wameainisha Mradi wa Makambako-Songea wa kV 220, ambao unaunganisha mikoa ya
Iringa, Njombe na Ruvuma km 250; naMradi wa North-East unaounganisha mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Kilimanjaro na Arusha. Aidha, mradi mwingine muhimu ni ule wa North-West, ambao unaunganisha mikoa ya Mbeya, Katavi, Rukwa na Kigoma.

Na kuhusu kusambaza nishati zaidi ya umeme vijijini, CCM inaanisha mkakati wa kuanzisha REA Awamu ya Tatu (REA-III) itakayokuwa na lengo pana la kuendeleza kazi nzuri iliyofanywa sasa lakini pia kuunganisha vijiji zaidi huku mkazo ukiwekwa katika shule, zahanati na vyanzo vya maji.

Hili ni eneo jingine ambalo kama kweli mtu anahitaji kuona Ilani ya mabadiliko Ukawa wamepoteza pointi tatu kabla ya mechi kuanza. Wamezipoteza. Hakuna namna nyingine zaidi ya kujifunza katika hili.
Mambo ya Nje
Vyama vyote vimezungumzia Sera ya Mambo ya Nje kwa minajili ya kuendeleza uhusiano wa kimataifa na kikanda. CCM wamesisitizia kuendeleza sera ya diplomasia ya uchumi ambayo ni Sera ya Kitaifa.
Ukawa wameahidi kitu ambacho kimatamko hakipo katika Sera yoyote ya Kitaifa; wanaita Ushirikiano wa Kimataifa Wenye Tija; sera hii mpya haijafafanuliwa popote kama inatofauti gani nay a sasa ya Kitaifa.
Lakini ukisoma ahadi za ndani ya ilani utabaini kuwa wananchoahidi Ukawa kimsingi hakina kipya zaidi ya kutekeleza matamko yale yale ya sera za sasa ambayo Tanzania imekuwa ikiyapigania sana kimataifa.
Hata hivyo moja ya mambo katika uchambuzi wa Ukawa ambayo yanaonesha hawakuwa na mchambuzi makini katika masuala ya kimataifa ni pale sera yao katika uchambuzi wa “Hali Halisi” inapoonekana kulaumu kuwa Tanzania ni kama vile imepoteza ushawishi Kimataifa.
Nikiri, mimi si mwanadiplomasia wala mwanataaluma katika hili, lakini nipo katika jiji hili la kitovu cha siasa na diplomasia za Afrika nimestushwa na tamko hilo. Kwanza tukubaliane kwamba siasa za sasa na jiografia yake (geopolitics) si kama za miaka 20 iliyopita na wala 40 iliyopita.
Ukisoma siasa za misimamo za enzi za vita Baridi nitakubaliana nawe kuwa Tanzania nayo ilipaza sauti yake sana zama hizo. Siasa za sasa kimataifa baada ya mageuzi ya Urusi na ujio wa sera na ubia mpya wa kiuchumi duniani zina namna yake ya kuzienenda katika masuala ya kimataifa na kikanda.
Tanzania katika uwanda huu iko juu sana na inaheshimika dunia na nikiwa nje ya Tanzania naweza kuthibitisha hili pasi na shaka. Mfano Tanzania licha ya kushika uenyekiti wa AU na taasisi zake kadha kama vile NEPAD, APRM, Baraza la Usalama n.k hata UN katika sauti kutoka Afrika zinazosikilizwa sana ni Tanzania.
Tanzania imeongoza masuala mbalimbali ya kikanda kama vile kushika uenyekiti wa Kamati ya AU kuhusu Majadiliano na Dunia katika masuala ya tabia nchi. Tumepata wenyeji kwa maana ya kuwa makao makuu ya Mahakama ya Africa, ICTR, Taasisi ya Rushwa Afrika (Africa Anti-Corruption Advisory Board) na tumeshika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa UN kwa miaka mitano na nusu.
Kama nchi tumepokea ziara rasmi za Marais na viongozi wote wakubwa duniani kutoka nchi zote zenye nguvu kama Marais wa Marekani, China, Ujerumani, Katibu Mkuu wa UNn.k. Diplomasia hii huwezi kuibeza hivi hivi kwa mtu anayefahamujiopolitiki, sanaa na sayansi za masuala ya kimataifa.
Kwa hiyo kiuchambuzi, na nikihitimisha kwa maana ya leo, niseme tu sehemu kubwa ya Ilani ya Ukawa haijitoshelezi kwa maana ya kuonesha ahadi mbadala, utekelezaji mbadala wa mambo wanayodhani CCM imekosea kuyafanya.
Badala yake kama neno mabadiliko linamaa sana ni Ilani ya CCM inayoonesha zaidi ahadi za mabadiliko si tu kwa minajili ya kuahidi, bali namna Ilani inavyofanya uchambuzi, inavyokwenda mbele na kuweka mfumo unaoonekana wa kutekeleza na zaidi kumpa mwananchi uwezo wa kuipima ahadi hizo miaka mitano ijayo kwa kuanisha malengo yanayopimika ya ahadi.
Ni kwa minajili hii basi ndio maana anuani ya makala haya inahoji na wiki ijayo itaendelea kuhoji tena “Tunatoa ahadi zinazopimika au orodha ya matumaini?”
Alamsiki.

*Mwandishi wa makala haya ni Mtanzania anayefanyakazi katika moja ya taasisi za kimataifa jijini Addis Ababa, Ethiopia. Kitaaluma ni mtafiti katika masuala ya siasa na maendeleo.