BIBI mmoja anayeonekana kula chumvi nyingi, Jumapili iliyopita alijikuta akiangua kilio baada ya kuzuiwa kuzungumza na Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Pombe Magufuli katika Uwanja wa Kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara, lakini alimsifia kiongozi huyo na kudai ndiye anayefaa kuiongoza Tanzania baada ya Rais Jakaya Kikwete.
Baada ya juhudi zake kushindikana, bibi huyo alianza kuangua kilio huku akisema alikuwa na ujumbe muhimu kwa mgombea huyo anayeamini ndiye rais ajaye na mkombozi wa kweli katika uongozi wa taifa hili.
“Huyu ndiye rais wetu anayetakiwa, naomba mniachie nikazungumze naye maneno machache nina jambo muhimu sana la kumwambia,” alisema bibi huyo akimuambia askari polisi aliyekuwa mbele yake ambaye hakumjibu lolote zaidi ya kumuangalia ‘kikauzu’.
Magufuli alikuwa akifanya kampeni hizo akitokea mkoani Singida ambapo alipita katika vijiji kadhaa na kurudi mkoani Dodoma katika wilaya mpya ya Chemba na baadaye alikwenda Kondoa hadi Babati mkoani Manyara ambako alifanya mkutano uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi.
Akiwa kwenye kampeni hizo, mgombea huyo aliwaahidi wakazi hao kuwaondolea tatizo sugu la maji, kusambaza umeme vijijini, kujenga hospitali ya rufaa kila mkoa na kuanzisha viwanda katika vijiji kulingana na malighafi inayopatikana eneo husika.