Waandishi wa habari wakifanya mahojiano na wakili wa serikali, Dk.Tulia Ackson mara baada ya kuahirishwa kesi hiyo katika Mahakama Kuu jana.
Wakili wa serikali Dk.Tulia Ackson akifanya mahojiano na wanahabari jana.
Wakili Peter Kibatala wa upande wa mlalamikaji akitoka katika chumba cha mahakama kwenye kesi hiyo hapo jana.
JANA, mawakili wa serikali zaidi ya sita wakiongozwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa serikali, Dk.Tulia Ackson walikuwa katika mvutano mkubwa na mawakili wa utetezi juu ya shauri la tafsiri ya sheria ya Uchaguzi Mkuu unaotaka wapiga kura kukaa umbali wa mita 200 baada ya kupiga kura, shauri lililoendelea katika Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam.
Majaji Sakieti Kihiyo, Aloysius Mjulizi na Lugano Mwandambo, wa Mahakama Kuu, walitumia siku nzima kusikiliza hoja za kisheria kuhusu shauri la katiba lililofunguliwa na Mgombea Ubunge Viti Maalumu jimbo la Kilombero (Chadema), Amy Kibatala, akitaka mahakama hiyo itoe tafsiri sahihi ya kifungu cha 104 (1) cha sheria ya Taifa ya Uchaguzi.
Mawakili kwa upande wa mlalamikaji waliokuwa wakijibu hoja zilizowasilishwa mahakamani hapo , ni Peter Kibatala aliyeanza kutoa hoja zake kwa kuiomba Mahakama iangalie na kutoa tamko kuhusu maana halisi na kusudio la kisheria la kifungu cha 104 (1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, sura ya 343 kama wananchi baada ya kupiga kura wanaruhusiwa kukaa kwa utulivu umbali wa mita 200.
Katika hoja zake Kibatala alisema msingi wa shauri hilo ni tamko la NEC lililotangazwa kwenye vyombo vya habari kuwataka wananchi kukaa umbali wa mita 200 kutoka sehemu ya kupigia kura.
Wakili wa serikali Dk.Tulia Ackson alisema idadi ya watu waliojiandikisha kupiga kura ni 22,751292 kwa Tanzania Bara hivyo kutokana na mwenendo wa siasa ambapo watu wamekuwa na mwamko, idadi hiyo ni kubwa ukilinganisha na mazingira ya kupigia kura na makazi ya watu kuweza kukaa kwa utulivu wakisubiri kumalizika kwa kupiga kura. Hivyo kusisitiza maelekezo ya NEC kuwa sahihi.
Aidha Jaji Lugano alimtaka Dk.Ackson kuisoma ibara ya 74 ya katiba ya Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania kifungu cha 12 ambapo baada ya kusomwa, Jaji aliendelea kuwauliza mawakili wa pande zote juu ya ibara hiyo.
Kesi hiyo inaendelea leo ambapo inatarajiwa kuwa maelekezo maalum yatatolewa tayari kwa matumizi wakati wa zoezi la kupiga kura keshokutwa Jumapili.