Saturday, October 31, 2015

Tamko: CUF yaipa ZEC siku tatu kukamilisha mchakato wa uchaguzi ........Isipofanya Hivyo Wananchi Wataamua Wenyewwe


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesema hakuna malalamiko yoyote yaliyowasilishwa katika siku ya upigaji kura.

Maalim Seif ambaye ni Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF ametoa kauli hiyo baada ya kuwepo taarifa kuwa mawakala wa CCM wameitwa pamoja na maofisa wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) katika kiwanda cha Makonyo Wilaya ya Chake Chake, kwa ajili ya kujazishwa fomu za malalamiko ili ziweze kutumika kudai kuwa yalikuwepo malalamiko katika zoezi hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Chama hicho zilizoko Mtendeni Mjini Zanzibar, Maalim Seif amesema njama hizo za CCM wameshazigundua na kawatozikubali.

Amesema njia pekee ya kuondosha utatanishi wa uchaguzi huo ni kukamilisha uhakiki wa majumuisho na kutangaza matokeo ya uchaguzi huo.

Amesema kwa upande wake pamoja na Chama chake, wataendeleza jitihada za kulipatia ufumbuzi suala hilo kwa kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa, ili kukamilisha uhakiki wa majumuisho ya kura kwa majimbo 14 yaliyobaki na hatimaye kutangazwa mshindi wa Urais si zaidi ya tarehe 02/11/2015.

Hata hivyo amesema iwapo hakutokuwa na hatua zozote zilizochukuliwa kukamilisha uchaguzi huo na kuheshimu maamuzi ya wananchi walio wengi hadi ifikapo tarehe 01/11/2015, viongozi wa CUF wataondoa mkono wao na kuwaachia wananchi waweze kutafuta haki yao kwa njia za amani.

Katika hatua nyengine Maalim Seif ameelezea kusikitishwa na vitendo vinavyofanywa na vikosi vya ulinzi na usalama kwa kuwatesa na kuwapiga raia wasiokuwa na hatia katika makaazi yao.

Amesema matukio hayo yamekuwa yakiripotiwa zaidi katika Wilaya za Magharibi “A na B”, na katika tukio la hivi karibuni amesema nyumba za raia wasiokuwa na hatia zimechomwa moto katika kisiwa cha Tumbatu na kuwafanya wananchi kuanza kupoteza uvumilivu.