Kasi ya utendaji kazi aliyoanza nayo Rais John Magufuli katika muda wa siku 20 inaonekana kubwa na ya aina yake lakini hivyo ndivyo ilikuwa kwa mtangulizi wake, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, miaka 10 iliyopita.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kwamba katika muda wa siku 20, tangu alipoapishwa Novemba 5, Rais Magufuli amekonga nyoyo za Watanzania baada ya kufanya ziara za kushtukiza Wizara ya Fedha na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, akavunja Bodi ya Wakurugenzi ya Muhimbili na kuzuia fedha kutumika kwa ajili ya sherehe badala yake akaagiza zifanye shughuli za jamii.
Halafu alitembelea Wizara ya Elimu ya Ufundi ambako aliagiza mitaala ya zamani irejeshwe, kisha akatembelea Wizara ya Miundombinu.
Novemba 20 Dk Magufuli alifanya mambo mawili mjini Dodoma; kwanza, asubuhi katika ikulu ndogo ya Chamwino alimuapisha Majaliwa kuwa Waziri Mkuu, na pili jioni, alilihutubia Bunge. Pamoja na uzuri wa hotuba yake alisusiwa na wabunge wa upinzani waliokuwa wanapinga Rais Magufuli kuingia bungeni Dk Ali Mohamed Shein kwa madai si rais halali wa Zanzibar.
Desemba 30, 2005 Kikwete alifanya kazi mbili; kwanza, asubuhi alimuapisha Lowassa kuwa Waziri Mkuu, na pili jioni alilihutubia Bunge. Hotuba yake ilipokewa kwa shangwe kwa vile alisisitiza kaulimbiu yake ya Maisha Bora kwa Kila Mtanzania, kuwapa ajira vijana na utayari wake kumaliza mpasuko wa kisiasa Zanzibar.
Hotuba za viongozi hao kwa kiasi kikubwa zilionyesha utayari wa kuwahudumia wananchi bila kujali itikadi za vyama, kupiga vita ufisadi, kupambana na majangili na wauzaji dawa za kulevya na kwamba lengo ni kuhakikisha Tanzania inasonga mbele kimaendeleo.
Moja ya hatua alizochukua na kumpa sifa Kikwete katika siku za mwanzo Ikulu ni kundwa kwa Tume Maalum iliyoongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu, Musa Kipenka iliyopewa kazi ya kuchunguza chanzo cha vifo na waliohusika na mauaji ya waliokuwa wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge wilayani Ulanga, Morogoro na dereva teksi mmoja wa Dar es Salaam. Tume hiyo iliundwa Januari 23 na ilipewa siku 21 kukamilisha kazi.