Tuesday, November 3, 2015

Lowassa Aandaa Mkakati Mzito!

Aliyekuwa mgombea urais wa Tanzania kwa Chama cha Demkrasia na Maendeleo (Chadema).
Na Waandishi Wetu
MAPYA! Kuna madai kwamba, aliyekuwa mgombea urais wa Tanzania kwa Chama cha Demkrasia na Maendeleo (Chadema) akiungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa (pichani) na viongozi wa chama hicho, wapo kwenye mkakati mzito wa kuvuna wanachama wengi kwa ajili ya uchaguzi ujao, Uwazi limeambiwa.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, Lowassa ameamua kujipanga upya kwa ajili ya maandalizi ya kutwaa urais kwenye uchaguzi wa Oktoba mwaka 2020.
MKAKATI
“Chadema na mgombea wake wa mwaka huu, Edward Lowassa wamepanga kuanzia mwakani watafanya mikutano katika kila kijiji, kila kata, kila tarafa, kila wilaya na kila mkoa. Lengo ni kuhakikisha chama kinavuna wanachama wengi kupita Chama Cha Mapinduzi (CCM),” kilisema chanzo hicho.
KILICHOBAINIKA
Chanzo kikazidi kusema kuwa, Chadema wameamua kufanya hivyo baada ya kubaini kwamba, CCM imekuwa ikijivunia wanachama wengi na kujiimarisha kwao mpaka vijijini nchini kote jambo ambalo na wao hawalishindwi.
“Unajua kuna vijiji ilibainika hata hawajui kama nchi ina vyama vingi. Lakini CCM wanaijua. Hii ndiyo imesababisha Lowassa aanze mikakati mizito mapema. Na si unamjua jamaa alivyo na mikakati,” kilisema chanzo.
HESABU YA LOWASSA
Chanzo tena: “Lowassa na chama chake hawahesabu kwamba bado miaka mitano kufikia uchaguzi wa mwaka 2020. Wao wanahesabu bado miaka mitatu tu.“Unajua kwa nini? Tayari mwaka huu unaisha. Tunaanza 2016. Kwa hiyo wao wanaanzia 2017, halafu 2018 kisha 2019. Ule mwaka wa 2020 hawauweki kwenye mahesabu kwa vile tangu Januari yake itakuwa ni mikakati ya kuelekea uchaguzi mkuu.”
WAFUASI WAPONGEZA
Uwazi juzi lilizungumza na baadhi ya wafuasi wa chama hicho na kuwauliza maoni yao kama chama kina mkakati huo wa kijiji kwa kijiji, wilaya kwa wilaya na mkoa kwa mkoa, wengi walipongeza sana wakisema CCM lazima ing’oke mwaka 2020.
“Mbona mkakati bomba sana huo. Hata mimi nina imani chama kitavuna wanachama wengi sana vijijini. CCM lazima wang’oke mwaka 2020,” alisema mmoja wa wanachama hao.
LOWASSA AFANYA KIKAO MAALUM DAR
Jumamosi iliyopita, Lowassa na baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho na wa Ukawa walifanya kikao maalum jijini Dar wakati wa chakula cha mchana kwa ajili ya kuzungumzia uchaguzi uliopita.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria hafla hiyo ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Tanzania Bara), Profesa Abdallah Safari, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Taifa na Mbunge Mteule wa Vunjo, James Mbatia na Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu.
Katika kikao hicho, Lowassa alisema:
“Nimefarijika sana, asanteni kwa msaada mlionipa. Sina cha kuwalipa. Ukweli ni kwamba kila mmoja alifanya kazi kwa nafasi yake.“Tujiandae kwa awamu ya pili na safari ndiyo imeanza. Unaweza kuchelewesha bahati ya mtu, lakini hauwezi kuiondoa.”
UWAZI NA AFISA HABARI WA CHADEMA
Baada ya taarifa hizo, Uwazi lilimtafuta Afisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene na kumuuliza kuhusu mikakati ya chama chake na Ukawa kwa ujumla baada ya uchaguzi kumalizika na CCM kuibuka washindi.
Makene alimsikiliza mwandishi mpaka mwisho, kisha akasema: “Kaka nipo kwenye kikao, nipigie baadaye.”
UWAZI NA NAIBU MKURUGENZI WA UCHAGUZI CUF
Baada ya kuachana na Makene ambaye alisikia kila kitu kutoka kwa mwandishi, Uwazi lilimtafuta Naibu Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Chama Cha Wananchi (Cuf), Shaweji Mketo na kumuuliza kuhusu mikakati hiyo.
“Mimi nawaunga mkono viongozi wa juu wa Chadema. Alichokisema Lowassa (kuhusu kujipanga upya) na Mbowe (Freeman) chama changu kinaunga mkono.”
ALICHOKISEMA MBOWE
Mketo aliunga mkono maneno ya Mbowe aliyoyasema kwenye mkutano huo maalum wa Jumamosi iliyopita. Alisema: “Siwezi kusema ulikuwa uchaguzi mgumu, bali ilikuwa ni vita. Tunachofanya, tunarudi nyuma, tunajipanga kukata rufaa kupinga matokeo katika majimbo zaidi ya 30.
UWAZI NA NAPE NNAUYE
Baadaye, Uwazi lilimsaka Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye.
“Sisi kama chama uchaguzi umekwisha. Tunakubaliana na Tume ya Uchaguzi kwamba ulikuwa huru na haki. Tunachosubiri sasa ni kuapishwa Rais Mteule, Dk. John Magufuli, Novemba 5, mwaka huu. Watanzania sasa tufanye kazi.” Habari hii imeandaliwa: Makongoro Oging’ na Haruni Sanchawa