POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imepiga marufuku maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), yaliyopangwa kufanyika bila ukomo kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni kinyume cha sheria.
Kamanda wa Kanda hiyo, Suleiman Kova aliwaambia waandishi wa habari jana ofisini kwake, jijini Dar es Salaam, kwamba maandamano hayo yana viashiria vya uvunjifu wa amani.
Maandamano hayo yaliyotajwa kuwa hayana kikomo, yalipangwa kufanyika katika maeneo yote ya jiji la Dar es Salaam. Kova alisema kama yakiruhusiwa, yatakuwa chanzo cha mfarakano mkubwa nchini, jambo ambalo litaathiri amani na maisha ya Watanzania.
Alisema maandamano hayo ni jambo ambalo haliwezekani, kwani pia yatasababisha msongamano mkubwa kwa wakazi wa jiji hilo na watapata usumbufu kwa kushindwa kufanya shughuli zao kwa ufasaha.
Alisema walipokea barua yenye Kumbukumbu namba CDM/PW/ GEN/042/2015 iliyoandikwa Oktoba 31, lakini iliwasilishwa ofisini kwake jana, ikitoa taarifa ya kufanya maandamano leo.
“Katika barua hiyo, Chadema Kanda ya Pwani walitoa taarifa ya kufanya maandamano ya amani yasiyo na kikomo kuanzia kesho (leo) katika maeneo yote ya jiji la Dar es Salaam kupinga kile walichodai ni uporwaji wa demokrasia dhidi ya mgombea wao wa urais Edward Lowassa ambaye wamedai ndiye mshindi,” alisema Kova.
Alisema baada ya kusoma barua hiyo kwa makini na kutafakari, amebaini kuwa kutokana na Sheria ya Polisi na Polisi Wasaidizi Sura ya 322 Kifungu cha 43 (1) kama ilivyorekebishwa mwaka 2002, taarifa ya maandamano inatakaiwa itolewe saa 48 kabla ya muda wa kuanza maandamano, kitu ambacho kimekiukwa, kwani barua hiyo ilipelekwa ofisini kwake jana.
“Kwa mujibu wa sheria hii, Chadema hawataruhusiwa kufanya maandamano hayo kutokana na kuchelewa kutoa taarifa kwa wakati. Wamemtaja Lowassa kuwa ndiyo mshindi, lakini kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Mwaka 1977, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ndiyo ina mamlaka ya kumtangaza mshindi,” alisema.
Alisema maandamano hayo ni batili na ni kinyume cha Sheria. Alisema kama hawakuridhika na uamuzi huo wa polisi, wanaruhusiwa kukata rufaa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi chini ya Kifungu Namba 43 (6) ya Sheria za Polisi na Polisi Wasaidizi Sura ya 322.
Hata hivyo, Kova alisema barua hiyo iliyowasilishwa na Chadema imeandikwa huku ikitawaliwa na shari; na pia inaonekana taarifa hiyo lengo lake ni kuvuruga amani.
“Nawaomba viongozi wa Chadema watumie busara, wasitake kuiingiza hii nchi katika matatizo na umwagaji damu, Watanzania sisi ni watu wa amani, hatujazoea haya mambo. Kuna taratibu na sheria wazifuate hizo,” alisema.
Alisema polisi wamejipanga vizuri kuhakikisha nchi inakuwa salama na atakayekaidi agizo hilo, atachukuliwa hatua kali za kisheria. Pia, alitaka vijana wasikubali kutumiwa katika kuvuruga amani.