MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, imemhukumu askari polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, G 9762 PC Daniel (24) kutumikia kifungo cha maisha jela, baada ya kupatikana na makosa ya kubaka na kumlawiti mtoto wa miaka 13.
Mbali na kifungo hicho, mtuhumiwa huyo ameamriwa kulipa fidia ya Sh milioni 2 ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Said Mkasiwa baada ya kukamilika ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo na upande wa mashtaka uliokuwa na mashahidi wanne.
“Mahakama inatoa hukumu kwa mtuhumiwa kutumikia kifungo cha miaka 30 kwa kosa la kubaka na kutumikia kifungo cha maisha jela kwa kosa la kulawiti mtoto na baadaye atalipa fidia ya Sh 2,000,000 ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizo,” alisema Mkasiwa.
Katika utetezi wake, mtuhumiwa kupitia kwa wakili wake ambaye alitajwa kwa jina moja la Manzi, alidai kosa hilo ni la kwanza na ni kijana mdogo ambaye ni nguvu kazi ya taifa, pia alifanya kosa hilo akiwa amelewa, hivyo hakujua alichokuwa akikifanya.
Awali Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Elik Shija, alidai hakukuwa na kumbukumbu za makosa ya nyuma dhidi ya mshtakiwa, hivyo aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mtuhumiwa ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.