Saturday, January 23, 2016

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Atangaza Rasmi Tarehe ya Kurudiwa kwa Uchaguzi Mkuu


TUME ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imetangaza kwamba uchaguzi wa marudio utafanyika Machi 20 mwaka huu na kuwataka wagombea wote walioshiriki katika uchaguzi uliofutwa wa Oktoba 25 mwaka jana, kujiandaa kushiriki uchaguzi huo.

Mwenyekiti wa Zec, Jecha Salim Jecha ametoa tamko hilo leo na kuongeza kuwa uchaguzi huo, utahusu nafasi ya Rais wa Zanzibar, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi pamoja na masheha.

Akifafanua zaidi, Jecha amevitaka vyama vya siasa kujiandaa na uchaguzi wa marudio, ambao unatokana na uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana uliofutwa baada ya kujitokeza kwa kasoro mbali mbali ambazo zilibainisha wazi wazi kwamba uchaguzi huo usingekuwa huru na wa haki.

Kutokana na kasoro hizo ambazo zingeweza kuibua malalamiko mbali mbali zilizosababisha kufutwa kwa uchaguzi huo, Jecha amewataka wagombea wote walioshiriki katika uchaguzi uliofutwa kujiandaa tena.

“Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec) inawatangazia wananchi wote kwamba uchaguzi wa marudio utafanyika Machi 20 na hii inatokana na kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana, baada ya kujitokeza wa kasoro mbali mbali ambazo ziliufanya uchaguzi huo sio huru tena,” amesema Jecha.

Aidha Jecha amesema kwamba katika uchaguzi wa marudio, hakutakuwa na uteuzi mwingine kwa wagombea wa nafasi zote ikiwemo urais, ujumbe wa Baraza la Wawakilishi pamoja na masheha, bali watatumia wagombea wa uchaguzi uliofutwa.

Mbali na wagombea, Mwenyekiti huyo wa Zec pia amesema hakutakuwa na mikutano ya kampeni za uchaguzi kama ilivyokuwa kwa Uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana.

“Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec) inawataka viongozi wa vyama vya siasa pamoja na wagombea wake na wananchi kwa ujumla, kujitayarisha na uchaguzi wa marudio utakaofanyika Machi 20. 

“Wananchi watapiga kura ya rais, uwakilishi pamoja na masheha ambapo katika kipindi hicho hakutakuwa na uteuzi wa wagombea wapya bali wale wale walioshiriki katika uchaguzi wa Oktoba 25 ndio watakaotambuliwa,” amesema.

Jecha amewapongeza wananchi wote wa Zanzibar kwa kudumisha amani na utulivu wa hali ya juu, katika kipindi chote kuanzia kampeni za kisiasa zilizohusisha mikutano ya kisiasa Unguja na Pemba, siku ya kupiga kura pamoja na kusubiri matokeo ya uchaguzi, ambapo hata hivyo matokeo hayo yalifutwa baada ya kubainika kujitokeza kwa kasoro mbali mbali.

Amesema utulivu uliooneshwa na wananchi katika kipindi cha uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana, unatakiwa kuendelea tena katika kipindi chote kuanzia kupiga kura na kusubiri matokeo na viongozi wa vyama vya siasa wametakiwa kuchunga kauli zao kwa ajili ya kuleta amani na kuepuka vitendo vya uvunjifu wa amani.

Zec ilifuta Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana baada ya kujitokeza kwa kasoro hizo, ikiwemo baadhi ya wagombea kutangaza matokeo ya urais katika vituo vya kupigia kura kwa kufanya majumuisho, kinyume na sheria ambayo imeelekeza kuwa mamlaka hayo ni ya Zec pekee.