Monday, January 11, 2016

Ofm yashuhudia live mgonjwa akifa mapokezi

P1300734
Ndugu wa marehemu wakilia kwa simanzi kubwa.
Stori: OFM, WIKIENDA
Morogoro: Inauma sana! Kile Kikosi cha Oparesheni Fichua Maovu (OFM) cha Global Publishers, imenasa tukio baya katika kufanya kwake kazi baada ya kushuhudia ‘live’ mgonjwa akifa kwenye mapokezi ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro huku manesi na wahudumu wakiingia matatani kwa uzembe.
Kabla ya tukio hilo la mwishoni mwa wiki iliyopita, kwa muda mrefu OFM imepokea kero juu ya mapokezi hiyo kuwa huwa kuna ucheleweshwaji wa kupokea wagonjwa hata wale wanaohitaji huduma ya dharura (emergency) hivyo kuamua kufanya uchunguzi kwa kuweka kambi na kubaini kuwepo kwa ukweli wa kero hiyo.
Katika siku zake kadhaa za kuweka ‘patroo’ eneo hilo, OFM ilishuhudia wagonjwa wakilalamika kucheleweshwa kupokelewa lakini hakukuwa na madhara ya mtu kupoteza uhai hadi ilipotokea kwa Moshi Mwandeme (30), mkazi wa wilayani Kilosa aliyekuwa amelazwa kwenye Hospitali ya Wilaya ya Kilosa akisumbuliwa na maradhi ya kubabuka mwili kwa kula samaki waliomdhuru.
P1300750
Muonekano wa hospitali hiyo.
Wakati OFM ikiwa kazini ilimshuhudia Mwandeme akifikishwa hospitalini hapo akiwa mahututi baada ya uongozi wa Hospitali ya Wilaya ya Kilosa kumpa rufaa ya kuletwa hospitalini hapo kwa gari la wagonjwa (ambulance) la wilaya.
Bila kujionesha kuwa ilikuwa ikifuatilia tukio hilo, baada ya umauti kumfika Mwandeme, OFM ilimpa nafasi mama wa marehemu, Khadija Abdallah ili kusimulia kilichotokea huku akirekodiwa sauti.
Kwa mujibu wa mzazi huyo, walipofika mapokezi walikaa na mgonjwa wao kwa zaidi ya saa moja bila huduma na kwamba walipomuuliza mhudumu wa zamu, aliwaambia kitanda cha kubeba wagonjwa ni kimoja hivyo wasuburi.
Huku akiangua kilio mama huyo alisimulia: “Tumesubiri kwa muda mrefu, mwanangu alikuwa akilalamika maumivu, mimi na dada yake, Zawadi Kheri na nesi tuliyekuja naye kutoka Kilosa, tulimshusha mgongwa kwenye ambulance na kumpeleka mapokezi.
“Ulipita muda mrefu sana, nesi tuliyekuja naye alikwenda tena kwa nesi wa zamu aliyekuwa mapokezi na kumwambia mgonjwa wetu amezidiwa hivyo wamuwahishe kumpa huduma lakini nesi huyo wa mapokezi alimjibu nesi wetu kuwa manesi wa vijijini washamba hawaelewi.
“Kauli hiyo ilimchefua nesi wetu na kujikuta akitokwa na machozi kwa hasira. Wakati tunambembeleza nesi huyo ndipo mwanangu akakata roho akiwa mapokezi na watu wakishuhuda.”
P1300733Hata hivyo, baada ya kutokea tukio hilo, baadhi ya watu walimshuhudia Mwandeme akifa walipiga kelele wakitaka kumshushia kichapo nesi huyo aliyekuwa mapokezi.
Baada ya kutokea kwa tukio hilo baya, ilibidi mwili wa marehemu uwekwe kwenye gari kurudishwa Kilosa kwa mazishi kwa kutumia ambulance iliyompeleka.
Baada ya kuibuka kwa kashfa hiyo nzito katika kipindi hiki ambacho Serikali ya Rais John Pombe Magufuli inatumbua majipu katika taasisi zake, OFM ilimtafuta Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Morogoro, Dk. Rita Lyamuya ili kuzungumzia kashfa hiyo ambapo awali aliwaka:
“Hivi ninyi siku zote mnaandika mabaya tu ya hospitali yetu? Kuhusu hilo tukio mimi ndiyo naingia ofisini sijapata taarifa hizo ngoja niende mapokezi nikaulize, nitakutafuta baada ya saa moja.”
mganga mkuuMganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Morogoro, Dk. Rita Lyamuya.
Saa moja baadaye, Dk. Rita aliwaita OFM ofisini kwake ambapo ilipofika ilimkuta na timu ya watu wanne ambapo daktari huyo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo:
“Baada ya kufuatilia nimegundua ni kweli kuna mgonjwa alifia mapokezi lakini kwa mujibu wa nesi wa zamu, mgonjwa huyo hakukaa zaidi ya saa moja pale mapokezi na hii inatokana na muuguzi kumhudumia mgonjwa wa kipindupindu aliyetangulia kufika.
“Tunao uchache wa vitendea kazi lakini naahidi tukio kama hili halitatokea tena.”