KATIKA kutambua na kuheshimu mchango wa straika, Mbwana Samatta kwa kutwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika kwa Wachezaji Wanaocheza Ndani, uongozi wa Dar Live kwa kushirikiana na viongozi wa Wilaya ya Temeke umeandaa sherehe ya kumpongeza staa huyo.
Sherehe hiyo itafanyika Jumanne, Januari 12, 2016 kwenye Uwanja wa Burudani wa Dar Live uliyopo Mbagala-Zakheem kuanzia mida ya 12:00 jioni kwa kiingilio kiduchu cha Tshs 5,000/=.
Samatta juzi aliandikisha rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kutwaa Tuzo ya Mchezaji Bora Afrika, alipowabwaga Robert Kidiaba (DR Congo) na Baghdad Bounedjah (Algeria).
Meneja wa Dar Live, Juma Mbizo ameliambia Championi Jumatatu kuwa wameratibu sherehe hiyo kwa kuwa Samatta ni ‘mtoto wa nyumbani’ ambako alizaliwa, kukulia na kusomea Mbagala, hivyo kulikuwa na kila sababu ya kumpongeza kwa heshima aliyowaletea.
“Tulikuwa na kila sababu ya kumuandalia sherehe. Amezaliwa, amekulia, amesomea, amechezea na familia yake yote iko Mbagala, hivyo lazima tumthamini. Lakini pia mashabiki watapa nafasi ya kupiga na tuzo hiyo pamoja na yeye,” alisema Mbizo.
Aliongeza sherehe hiyo itanogeshwa kwa burudani kutoka kwa Juma Nature, Bendi ya Twanga Pepeta, Msaga Sumu pamoja na Khalid Chokoraa ambaye atamtungia single yake ‘special’ kumpongeza kwa tuzo hiyo.
Pamoja na yote, pia viongozi wa Simba na Africa Lyon wamealikwa kwa mchango wao ambako Samatta alipata kuchezea kabla ya kutimkia Mazembe ambako ametwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika mbali na tuzo binafsi.
“Naomba watu wajitokeze kwa wingi kuonesha sote tuko pamoja na safari yake ya soka,” aliongeza Mbizo