Tuesday, February 9, 2016

Mrembo ababuka uso afariki dunia, chanzo ni samaki

Agnes Haule akiwa amebabuka usoni baada ya kula samaki.
Stori: Issa Mnally, UWAZI
DAR ES SALAAM: Inasikitisha sana! Mrembo aliyejulikana kwa jina la Agnes Haule (29) amefariki dunia kwa madai ya kula nyama ya samaki ikisemekana alikuwa na mzio (allergy) nazo.
Ilielezwa kuwa, mrembo huyo baada ya kula samaki, ambaye haijafahamika ni wa aina gani, alianza kuwashwa mwili mzima na kumsababishia kuvimba na ngozi kubabuka, akitokwa na vidonda, hasa sehemu za usoni.
Akizungumza na mwandishi wetu, mtoa habari mmoja (hakutaka jina lake liandikwe gazetini kwa vile si msemaji wa familia) alisema Agnes alikumbwa na mauti wiki iliyopita kwenye Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar baada ya kukimbizwa hapo kufuatia madhara hayo.
IMG-20160203-WA0002Agness enzi za uhai wake.
“Yaani ni jambo la kusikitisha, kushangaza na la ajabu sana kula samaki tu kukamtokea matatizo yale, ama kweli Mungu ana maajabu yake jamani,” alisema mtoa habari huyo. “Ninachofahamu mimi ni kuwa, unaweza ukala kitu kikakudhuru lakini hii ya kumsababishia mtu umauti ni ngumu sana, labda huyo samaki alikuwa na sumu.”
Msiba wa Agnes ulikuwa Mbezi ya Kimara jijini Dar huku mwili wake ukisafirishwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenda mkoani Ruvuma kwa mazishi.Uwazi, juzi lilimpigia simu dada wa Agnes ili kumsikia anasemaje kuhusu msiba huo lakini hakuwa tayari kuzungumzia lolote.
“Naomba mtuache. Sisi kama familia tumeumia sana na msiba huu, siwezi kusema lolote na hakuna anayeweza kusema lolote, mtuache,” alisema. Habari zaidi zilidai kuwa, marehemu Agnes alikuwa na ukaribu wa kawaida na bosi wa Kundi la Orijino Komedi, Sekione David ‘Seki’ ambapo pia aliwahi kuhudhuria ndoa yake mwaka jana. Alipopigiwa Seki na kuulizwa alisema:
“Da! Alikuwa rafiki yetu lakini mimi siwezi kusema lolote jamani.”
Kitaalam, mzio husababisha ugonjwa wa Anaphylaxis ambao huanza ghafla na huweza kusababisha kifo. Dalili kubwa ni upele wa kuwasha, kuvimba koo na shinikizo la chini la damu. Chanzo cha kawaida ni kuumwa na wadudu, vyakula na dawa.