Monday, February 22, 2016

Paul Makonda Na Meya Wa Kinondoni ( Chadema ) ' Washikana Mashati ' Kuhusu Mipaka Ya Kiutendaji

Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob na Mkuu wa wilaya hiyo, Paul Makonda wameingia kwenye mvutano kuhusu kuvuka mipaka ya utendaji wa halmashauri hiyo.

Mvutano huo umekuja baada ya Jacob kumtuhumu Makonda kuwa ametoa taarifa za kikao cha kamati za fedha ya halmashauri hiyo kilichofanyika wiki iliyopita kinyume na taratibu.

“…Tena hata kwenye kikao hakuwepo, lakini nashangaa kuona ameenda kutangaza kwenye vyombo vya habari kuwa Wilaya ya Kinondoni inatarajia kupata dola 300 milioni za Marekani sawa na Sh600 bilioni kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya miradi ya maendeleo,”alisema Jacob jana kwenye mkutano na waandishi wa habari.

“Vikao vyote vya halmashauri ni siri… huo ni upotoshaji na Makonda anaingilia mamlaka zisizokuwa za kwake, ” alisema.

Jacob alisema halmashauri hiyo imeshindwa kufumbia macho jambo hilo kwani linaweza kuleta mvutano baadaye.

“Mimi nalalamikiwa na wajumbe wa kamati, wanasema kwa nini taarifa za kikao ambazo ni za siri zinatangazwa wakati bado michakato yake inaendelea?” alihoji Jacob.

Meya huyo alisema Makonda ambaye alipewa taarifa hizo na maofisa tarafa waliohudhuria kikao hicho, alitakiwa kuuliza uongozi wa halmashauri kabla ya kutangaza kwa umma.

“Sasa leo ikitokea wajumbe wamegoma kupitisha maazimio kuhusu mchakato huo hizo hela atatoa wapi?” aliendelea kuhoji.

Alisema endapo Makonda ataendelea na tabia hiyo, maofisa tarafa watazuiliwa kuhudhuria kwenye vikao vya kamati za fedha za halmashauri hiyo.

Hata hivyo, Jacob alisema si mara ya kwanza kwa mkuu huyo wa wilaya kuvuka mipaka na kuingilia shughuli za halmashauri, ambazo kimsingi zinapaswa kufanywa na meya, mkurugenzi au msemaji wa halmashauri.

Meya huyo alisema mara ya kwanza Makonda alisema halmashauri itajenga machinjio ya kisasa, wakati anafahamu hana uwezo wa kupata fedha za kufanikisha mradi huo.

Jacob alisema halmashauri ndiyo yenye dhamana na kuidhinisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo.

Pili, aliwahi kuwaita wenyeviti wa Kinondoni Leaders Club kwa ajili ya kuzungumzia mchakato wa kuvunja maeneo ya wazi yaliyojengwa.

Alipotafutwa Makonda kueleza kuhusu madai hayo, alisema Jacob bado ni mwanafunzi hivyo hawezi kuzungumza chochote juu ya madai hayo.

“Amechaguliwa kuwa meya juzi tu bado mwanafunzi, hafahamu mipaka ya mamlaka yangu. Akijifunza na kuelewa hizo kelele hamtazisikia tena,” alisema Makonda