Saturday, March 26, 2016

Al Ahly hali tete Misri

MMG25643Timu ya Al Ahly ya Misri .
Mwandishi Wetu,
Cairo
UKIACHANA na kukosa video za mechi za Yanga za hivi karibuni, Al Ahly inapambana kuhakikisha inakuwa vizuri kabla ya Aprili 9, mwaka huu itakapocheza na Wanajangwani hao.
Yanga itacheza na Al Ahly ya Misri katika mchezo wa kwanza wa 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kisha kurudiana wiki moja baadaye.
Mkurugenzi wa Michezo wa Al Ahly, Syed Abdul Hafiz, amesema timu yake imepata ugumu kuelekea mchezo huo baada ya kushindwa kupata video za Yanga katika mechi zake mbili za mwisho dhidi ya APR.
cercle-yangaWachezaji wa timu ya Yanga.
“Ubalozi wetu (wa Misri) nchini Tanzania umetuthibitishia kwamba mechi ya Yanga na APR haikuonyeshwa na televisheni yoyote ile, hivyo hatuwezi kupata video ya mechi hiyo.
“Sasa tunatafuta video ya mechi yao ya kwanza iliyochezwa Rwanda na tumemuagiza ofisa ubalozi wetu kule atupe hiyo video, tunachotaka ni video ya mechi za mwisho za Yanga,” alisema Hafiz.
Katika raundi ya kwanza ya ligi hiyo, Yanga iliitoa APR kwa mabao 3-2, kwanza ilishinda mabao 2-1 Kigali, Rwanda kisha ikatoka sare ya bao 1-1 jijini Dar es Salaam.
GOMAA HALI TETE
Nyota wa Al Ahly, Saleh Gomaa ameanza mazoezi akitoka katika majeraha ya misuli aliyopata katika mchezo dhidi ya Libolo Recreativo Angola, hata hivyo bado hakuna uhakika wa kucheza dhidi ya Yanga.
Daktari wa Al Ahly, Khalid Mahmood alisema Gomaa ameanza mazoezi mepesi katika kikosi cha kwanza na kucheza kwake mechi za ushindani itategemea na uamuzi wa kocha.
Katika msimu huu, Gomaa ameichezea Al Ahly mechi 13 kwa dakika 475 na kufunga mabao mawili akitengeneza matano, aliumia katika mchezo wa kwanza dhidi ya Libolo.
KOCHA SPURS ASITISHA MAZOEZI
Kocha wa Al Ahly, Martin Jol juzi Alhamisi alisitisha mazoezi ya viungo ya timu hiyo katika gym kwa muda kisha akawahamishia wachezaji mahali pengine kuendelea na mazoezi hayo.
Jol ambaye ni kocha wa zamani wa Tottenham Hotspur, alisitisha mazoezi hayo ili kusisitiza ukarabati wa gym hiyo uendane na hadhi ya klabu na mechi zilizo mbele yake ikiwemo dhidi ya Yanga.
Kocha huyo aliwapumzisha wachezaji wake jana na leo anatarajiwa kuendelea na mazoezi yake.