Thursday, March 31, 2016

DART Imejipanga Kuwatoa Wafanyabiashara Waliogeuza Masoko Kwenye Vituo Vya Abiria


Wafanyabiashara waliovamia miundombinu ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) na kuigeuza kuwa masoko ya bidhaa wametakiwa kuondoka ili kupisha mradi huo ambao unakaribia kuanza katika siku chache zijazo.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),  Suleiman Jaffo ametoa kauli hiyo wakati kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa TAMISEMI ilipotembelea ofisi za Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka jijini Dar es Salaam na kupokea taarifa za maendeleo ya mradi huo.

Amesema yapo mambo yanayokamilishwa ndani ya serikali na wadau wa mradi ikiwemo kufunga mfumo wa utozaji nauli kwa njia ya kadi na mengineyo hivyo amewaomba wananchi kuendelea kuwa na subira na kuahidi kuwa mradi huo utaanza hivi karibuni na utatoa huduma nzuri ya usafiri kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam, huku Kaimu Mtendaji mkuu  wa DART Ronald Lwakatare akitoa rai kwa wananchi kuhakikisha miundombinu ya mradi huo inatunzwa dhidi ya uharibifu.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa DART, Bw. Ronald Lwakatare amesema  Wakala umejipanga kutoa huduma hiyo huku akiwaomba wananchi kuendelea kuitunza miundombinu yao ili isiharibiwe na watu wasiowaaminifu.