Madai hayo aliyatoa Alhamisi iliyopita baada ya gazeti hili kumuuliza habari zilizoenea kwamba, amemuangukia Wastara akitaka warudiane kwani yaliyopita si ndwele.
Sadifa alisema kuwa, aligundua hilo la kurogwa baada ya Wastara kuondoka nyumbani kwake na kutangaza kwenye vyombo vya habari kuwa, amepewa talaka mbili.
Akizungumza kwa dakika 25, Sadifa alikwenda mbele zaidi kwa kusema: “Ukimwangalia Wastara harakaharaka unaweza kusema ni mwema sana lakini hana wema wowote. Hivi Wastara ni wa kuniroga mimi kweli?”
ILIKUWA HIVI
Risasi Jumamosi: (baada ya kujitambulisha na salamu) “mheshimiwa tunataka kujua nini kinaendelea kati yako na mkeo Wastara?”Mume: “Kuhusu nini?”
Risasi Jumamosi: “Kuna madai kwamba, umeamua kumrudia na wiki iliyopita uliwapa gari mashemeji zako waende Morogoro kumfuata Wastara.”
Mume: “Kwanza hizo habari si za kweli. Mimi wale mashemeji zangu waliniomba gari wamfuate ndugu yao. Nilitoa kwa ubinadamu tu, nikawawekea na mafuta.”
AMTAJA RAFIKI WA SAJUKI
Risasi Jumamosi: “Lakini inadaiwa kuwa ulisema arudi mkae myamalize, ila kule Morogoro kwa yule babu yake, ikawa kazi kutoka, unasemaje kuhusu hilo?”
Mume: “Babu yake yupi?”
Risasi Jumamosi: “Yule Abdulaaziz Babu.”
Mume: “Yule si babu yake Wastara. Yule ni bwana’ake kama hamjui. Mimi juzi tu ndiyo baadhi ya ndugu zake wameniambia ukweli kwamba yule babu, si babu yao bali alikuwa rafiki mkubwa wa marehemu Sajuki (Juma Kilowoko, aliyekuwa mume wa Wastara).”
ASEMA AMEMCHUKULIA MKE
Sadifa hakuishia hapo, aliendelea kumwanika Wastara hivi:
“Sasa wewe jiulize, mkeo mnagombana, anakwenda kwa rafiki wa marehemu mume wake. Kwa nini asiende kwao? Kule anakaa kufanya nini? Yule Babu ndiye amenirithi mimi kwa Wastara.”
AFUNGUKA ZAIDI
“Kuna wakati fulani Wastara aliumwa, dokta akamwambia atulie kwa muda asitembeetembee. Kesho yake akaniambia anakwenda Morogoro kwa huyo babu yake. Nilimkatalia, akalazimisha, akaenda. Sasa mke anawezaje kwenda mahali bila ridhaa ya mumewe?
“Alipokuwa kule, nikawa nampigia simu hapokei kwa muda wa siku tatu. Siku moja nyumbani alikuja kijana wake anayemfanyia biashara, nikamwambia Wastara yupo Morogoro, akampigia simu mbele yangu, akapokea, wakaongea. Walipomaliza, mimi nikampigia, hakupokea!”
BABU ALIOMBA PESA KWA MUME“Basi, siku hiyo huyo babu akanipigia simu, akasema eti Wastara anaumwa, mguu unatoka damu, nimtumie pesa ampeleke hospitali. Nikamwambia sina na hata kama ningekuwa nazo nisingetuma.
KUHUSU KUMROGA
“Hivi Wastara ni wa kuniroga mimi kweli?”
Risasi Jumamosi: “Kukuroga? Hayo sasa ni mambo ya imani mheshimiwa. We umejuaje kama anakuroga?”
Mume: “Niliambiwa na watu wawili, mmoja dereva wangu, mwingine ni kijana wangu. Tena hao wameniambia juzi tu baada ya mambo kuharibika.
ADAI KUTEGEWA KOMBE
“Wakasema kuna siku walikwenda na Wastara kwa huyo mganga. Wastara alikuwa na ndugu yake mmoja. Walipofika, vijana wangu hawakuingia. Kwa hiyo hawakujua walifuata nini! Mara ya pili akawaambia kuwa, wamekwenda pale kuchukua dawa eti ili isaidie ndoa yetu iwe na amani na mimi niache macho juujuu. Akapewa kombe kama unalijua kombe, aitie kwenye maji anipe ninywe.
“Sasa wale vijana wangu wakamshauri Wastara kwamba, kama maji hayo ya kombe atanipa yeye ninywe nikigundua itakuwa balaa, wakamwambia awape wao ndiyo wanipe mimi ninywe ili nikijua wataniambia ni dawa ya kukinga mwili. Lakini wao hawakunipa na wanayo mpaka leo (juzi, Alhamisi)!”
SIKU YA WASTARA KUONDOKA NYUMBANI
“Mimi sikuwahi kutoa talaka kama Wastara anavyoeneza hizi habari. Siku hiyo anaondoka nyumbani mimi nilikwenda kwenye kamati za bunge, wakati naingia akanipigia simu na kusema anataka tuongee.
“Nilimwambia tutaongea baadaye yeye akataka muda uleule, nikakataa. Akasema anachotaka yeye nimpe shilingi milioni kumi afanye biashara. Nikamwambia sina, ndiyo akaondoka. Sasa jamani, mkeo kama anataka pesa ukamwambia huna ndiyo aondoke nyumbani? Mimi naona alifuata pesa tu.”
KUHUSU TALAKA SASA
Sadifa alizungumzia talaka ambapo alisema: “Sasa ndiyo nimeamua kumpa talaka rasmi. Kesho (jana, Ijumaa) nitakwenda kwao kutoa talaka labda wakimbie.”
BAADA YA MUME, WASTARA HUYU HAPA
Baada ya Sadifa kutumia dakika 25 kumzungumzia Wastara, naye mwanadada huyo akatumia dakika 22 kujibu mapigo.
AANZA KWA MADAI YA KUROGA
Wastara alisema kuwa, anajua mwanaume huyo atasema mengi yakiwemo hayo ya kumroga, lakini..:
“Lakini mimi sijamroga wala sina mpango huo. Kama hao vijana wake wamemwambia hivyo, mbona vijana haohao waliwahi kuniambia kuwa, yeye amewatuma wampigie picha mahali ili aseme amenifumania. Mimi nilisema wapi!”
ANAPANGUA KUHUSU BABU
“Atasema mengi, mimi na babu hatuna chochote zaidi ya kuwa mtu wa karibu. Yeye ana mangapi mimi sijasema. Mbona anakunywaga sana pombe.”
SH. MILIONI KUMI
“Kumuomba shilingi milioni kumi ni kweli. Na nilimwomba kwa kuwa ni mume wangu, sasa ningemuomba nani. Na ni pesa ambayo aliniahidi toka siku nyingi.”
KUMBE ALILAZIMISHWA KUOLEWA!
“Kwanza ngoja nikwambie, anaposema mimi nilifuata pesa kwake si kweli. Mimi nimeishi na Sajuki katika maisha ya umaskini, sasa leo naanzaje kufuata pesa kwa mtu. Ila mimi niliolewa kwa kulazimishwa, sikutaka kuolewa na yule bwana.”
IWE KWA WEMA
Madai ya pande zote ni mazito. Hata hivyo, gazeti hili litaendelea kufuatilia mwenendo wa wawili hao ili kujua mwisho wake. Lakini ushauri kwa wote ni kukaa chini na kuondoa tofauti zao ili hata kama ni kuachana iwe kwa wema na si kwa uhasama.
HUYU NI BABU
Gazeti hili juzi lilimpigia simu Babu ili kumsikia anasemaje kuhusu madai ya Sadifa. Yafuatayo ni maelezo yake:
“Kwanza nimecheka sana. Anaposema mimi nimemchukua mke wake aliniona nyumbani kwake? Kwanza akumbuke wakati wa kumuuguza Wastara hivi karibuni kwa nini aliniita nyumbani kwake? Kwa nini alikuwa akinipa gari nimpeleke Wastara hospitali?
“Wakati anaondoka kwenda Zanzibar kwenye vikao vyao vya ubunge kwa nini alikuwa ananiomba nimpeleke uwanja wa ndege (Dar)? Kama kweli yeye haniamini kwa nini alikuwa anafanya yote hayo?
“Akae chini na Wastara waongee wayamalize. Mbona madogo sana hayo! Asitumie ubunge wake kutisha watu. Kama anaamini mimi nimemchukua Wastara achukue hatua yoyote ile.”