Msanii Ali Kiba ambaye kwa sasa anafanya poa na kazi yake yaLupela amefunguka na kusema kuwa muda si mrefu kutoka sasa ataachia kazi nyingine mpya.
Msanii Ali Kiba akiwa studio za East Africa Radio kwenye kipindi chaPlanet Bongo amedai kuwa kazi yake hiyo anayotaka kuiachia mpaka sasa hana jina lake lakini atawaachia mashabiki ambao ndiyo watakuwa na jina la kazi hiyo.
“Mashabiki zangu kaeni mkao wa kula nashusha balaa lingine muda si mrefu kutoka sasa. Hii ngoma hata sijui mimi niiiteje yaani ila nitawaachia wenyewe wananchi mchague jina la kazi hiyo” alisema Ali Kiba.
Mbali na hilo Ali Kiba amesema kuwa kitendo chake cha kutoa wimbo bila video kimekuwa na athari kubwa kwake kwani wimbo unakuwa mkubwa na mashabiki wanakuwa tayari na video zao vichwani mwao, kiasi kwamba anapokuja kutoa video ya wimbo huo unakuwa tofauti na mategemeo na matarajio ya baadhi ya watu jambo ambalo huwa linaleta maneno maneno.