Saturday, April 2, 2016

Rais Magufuli Apiga Simu Clouds TV Na Kutaja Mshahara Wake Anaolipwa....Asema Akitoka Likizo Ataonyesha Nyaraka za Malipo


Rais John Magufuli analipwa Sh9.5 milioni kwa mwezi. Huo ndiyo mshahara ambao mkuu wa nchi ameutangaza kwa umma bila ya kutoa ufafanuzi kama unajumuisha marupurupu mengine kulingana na cheo chake.

Rais ameamua kuweka hadharani masilahi yake wakati kukiwa na mjadala mkubwa uliotokana na tamko lake alilolitoa mapema wiki hii kuwa atapunguza mishahara ya watendaji wakuu wa taasisi na mashirika ya umma kutoka Sh40 milioni hadi Sh15 milioni, akisema katika “Serikali ya Magufuli”, ambayo itadumu kwa miaka 10 iwapo atachaguliwa tena mwaka 2020, hakuna mtu atakayelipwa zaidi ya kiwango hicho.

Dk Magufuli, ambaye hivi sasa yuko nyumbani kwake Chato mkoani Geita kwa mapumziko aliamua kutangaza mshahara wake baada ya wabunge wawili, Zitto Kabwe (ACT Wazalendo) na Tundu Lissu (Chadema) kuripotiwa kutaka atangaze mshahara wake baada ya tamko la kupunguza mishahara ya vigogo wa mashirika hayo ya umma.

Wakati wa kipindi cha asubuhi cha 360 kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Clouds, watangazaji walisoma habari hiyo na kuanza kujadili mshahara wa Rais.

Wakati wakijadili ndipo Rais alipowapigia simu kuwatajia mshahara wake.

Meneja wa kipindi cha 360 ambacho hufanya uchambuzi wa magazeti, Hudson Kamoga alithibitisha kuwa Rais Magufuli alimpigia simu kumtajia mshahara wake.

“Aliniuliza kwa nini sikuwapo kwenye kipindi, nikamjibu kuwa nipo Arusha kwa majukumu mengine,” alisema Kamoga.

“Akaniambia niwaambie wenzangu ambao wapo kwenye kipindi kuwa mshahara wake wa mwezi ni Sh9.5 milioni na mshahara huo ameukuta na kwamba akirudi Dar es Salaam, twende ofisini kwake akatuonyeshe salary slip.” Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Gerson Msigwa alisema Ikulu hakuna mtu anayelipwa zaidi ya Sh9.5 milioni.

“Kwa hiyo kama Rais ameamua kuzungumza nao (Clouds) kuhusu mshahara wake, naomba asubiriwe akirudi Dar es Salaam akawaonyeshe salary slip yake kama atafikia hatua hiyo,” alisema Msigwa. Lakini uamuzi wake wa Rais kutangaza mshahara wake, umekosolewa na Lissu.

“Mshahara alioutangaza Rais unaendelea kuwaweka wananchi njiapanda kwa kuwa hauna uchanganuzi,” alisema Lissu alipoulizwa maoni yake kuhusu kiwango cha mshahara wa mkuu wa nchi.

“Anapaswa kueleza iwapo ni fedha ya jumla, marupurupu yapo humo ndani kwa sababu mshahara wa mbunge ni Sh3.6 milioni na anapohesabiwa marupurupu yake inafikia kiasi cha Sh12 milioni na hizi ndizo anazoondoka nazo.

“Sasa tunahitaji kujua kama ndiyo fedha anayokwenda nayo nyumbani au ni vinginevyo.”

Kabla ya Dk Magufuli kufanya hivyo, kumekuwa na mjadala kwa muda mrefu kuhusu mshahara wa Rais, na kila vyombo vya habari vilipojaribu kutaja, Ikulu ilikanusha mara moja lakini haikutoa ufafanuzi wa kiwango sahihi cha mshahara.

Mtandao wa African Review mwaka jana ulifanya uchambuzi wa mishahara ya marais Afrika na uliwataja marais watano wanaoongoza kwa kuwa na mishahara mikubwa kwa mwaka kuwa ni Paul Biya wa Cameroon anayelipwa dola 610,000 za Marekani, akifuatiwa na kiongozi wa Morocco, Mfalme Mohammed VI (dola 480,000) na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini (dola 272,000).

Katika orodha hiyo, Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete alishika nafasi ya nne akitajwa kupata dola 192,000 na wa tano alikuwa Rais Abdel Aziz Bouteflika wa Algeria, anayelipwa Dola168,000.

Madhumuni ya utafiti wa mtandao huo yalikuwa ni kuangalia kiasi wanacholipwa marais wa Afrika kwa mwaka na kile inachopata taifa husika kwa muda huo.

Pia walilenga kuangalia uhusiano wa viongozi na wananchi wa kawaida wanaowangoza.

Kwa mujibu wa mtandao huo, vyanzo vya taarifa za mishahara ya marais hao vilipatikana kutoka mitandao na wanahabari wa nchi husika. Habari hizo ziliporipotiwa, Ikulu ilikuja juu lakini haikutaja mshahara halisi wa Rais.