SERIKALI ya China imeiunga mkono serikali katika mkakati wake wa kutoa elimu bure, ikisisitiza kuwa chini ya uongozi wa Rais John Magufuli, Tanzania inasifika duniani.
Katika kuunga mkono elimu bure, ubalozi wa nchi hiyo nchini umetoa msaada wa madawati 400 yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 28 kwa shule mbalimbali za msingi katika wilaya ya Iramba mkoani Singida.
Balozi wa China hapa nchini, Dk Lu Youq’ng alisema msaada huo ni moja ya juhudi za nchi yake kuiunga mkono Serikali ya Tanzania katika kutoa elimu bure.
“Wakati mimi nimechangia madawati 300, Kampuni inayochimba madini hapa ya Sun Shine Group imechangia madawati 100 ili kuniunga mkono,” alifafanua.
“Wakati mimi nimechangia madawati 300, Kampuni inayochimba madini hapa ya Sun Shine Group imechangia madawati 100 ili kuniunga mkono,” alifafanua.
Akikabidhi madawati hayo katika mikutano mitatu tofauti kwenye mji wa Kiomboi, Shelui na Misigiri, Balozi Youq’ng alisisitiza umuhimu wa Tanzania kuwekeza kwenye elimu kuwaletea wananchi wake maendeleo ya kweli.
“Hata kama nchi ni maskini kiasi gani, lazima elimu itiliwe mkazo; tena iwe ni elimu bora na elimu bora haiwezi kuja kwa wanafunzi kukaa chini. “Madawati ni moja ya mambo ambayo yanamjengea mwanafunzi mazingira mazuri ya kujifunzia,” alisema.
Aliongeza, “kutokana na umuhimu huo, ndio maana mbunge wenu aliponijia na kuniomba msaada wa madawati, sikusita hata kidogo. Nilijua anafanya hivyo ili kuisaidia jamii yake kuboresha elimu”. Aliyeomba msaada huo ni Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba.
Aidha, balozi huyo amewapongeza wakazi wa mkoa wa Singida kwa kumchagua Dk Magufuli kuwa Rais na kuongeza kusema kuwa chini ya uongozi wake sasa Tanzania inasifika duniani kote. “Nitahakikisha nchi yangu inaendelea kusaidia maendeleo ya nchi hii kwa kuwa urafiki wetu ni wa enzi na enzi,” alisema.