Hofu ya ushirikina imetikisa Mkoa wa Arusha kufuatia tukio la hivi karibuni ambapo mwanafunzi wa Chuo cha Kompyuta jiji hapa, Witness Obed (21) aliyefariki dunia Aprili 12, mwaka huu na kuzikwa kwenye makaburi ya nyumbani kwao Kijiji cha Nanja, Kata ya Moshono wilayani Arumeru, Arusha kuibuka akiwa hai.
Binti huyo aliibuka kwao hivi karibuni akiwa mpole na kuwafanya baadhi ya watu, wakiwemo wazazi wake kutimua mbio kwa hofu.
Watu kutoka maeneo mbalimbali jijini hapa wamekuwa wakimiminika nyumbani kwa wazazi wa binti huyo kwa lengo la kumshuhudia kwa vile ndugu walishaamini kuwa, mpendwa wao huyo alishakufa na alizikwa.
UWAZI LATIA TIMU NYUMBANI
Baada ya kusikia taarifa hizo, Uwazi lilifunga safari mpaka eneo la tukio na kumshuhudia binti huyo kisha likaenda kwenye kaburi alilozikwa.
Kwenye kaburi hilo, msalaba wenye kuonesha siku yake ya kuzaliwa (1992) na kufa (12, Aprili, 2014) ulikuwa bado umesimama imara huku kaburi lenyewe likionesha dalili ya kutitia kidogo.
BABA MZAZI ASIMULIA
Akisimulia mkasa huo kwa mshangao mkubwa, baba mzazi wa binti huyo, Obed Leiyo alisema:
“Ilikuwa Aprili mwanzoni, binti yangu alitoweka nyumbani baada ya kurudi kutoka chuoni majira ya saa 2 usiku akiwa amechelewa.
“Mimi kama mzazi nilimfokea kwa kuchelewa kwake kurudi nyumbani.
“Yeye kwa hasira zake alizunguka nyumba akaondoka muda huohuo na hakurudi kabisa hapa nyumbani.
“Siku iliyofuata tulianza kumtafuta maeneo mbalimbali bila mafanikio, tukatoa matangazo kwenye vyombo vya habari lakini binti yangu hakuonekana.”
TAARIFA ZAFIKA, KAFA
Mzazi huyo aliendelea kusema: “Siku moja tulipata taarifa kwamba kuna mwili wa msichana umeonekana katika Kijiji cha Bwawani hapahapa Arumeru.
“Mimi pamoja na ndugu wengine tuliamua kwenda katika kile kijiji. Tulipofika tuliambiwa ni kweli mwili wa msichana uliokotwa lakini wananchi wakauzika.”
WAFUKUA KABURI
Baba huyo anaendelea: “Niliamua kwenda Kituo cha Polisi cha Usa River ambako niliomba kibali kwa ajili ya kufukua kaburi na kuutoa mwili ili kuutambua kama ni binti yangu au la!
MWILI WASAFIRISHWA, WAZIKWA
Baba huyo wa Witness alizidi kueleza kuwa waliusafirisha mwili huo hadi nyumbani kwake Moshono na kuandaa taratibu za mazishi ambapo Aprili 23, mwaka huu mwili ulizikwa.
AIBUKA GHAFLA
Hata hivyo, Obed anasema alishangaa siku ya tukio kumwona binti yake huyo akiibuka nyumbani hapo akiwa hai jambo ambalo lilimshangaza na kumfanya akimbie kwanza na baadaye kufanya mawasiliano naye.
BINTI ASIMULIA
Akizungumza na Uwazi, binti huyo alikiri kutoweka nyumbani kwao Aprili 15, mwaka huu na kwenda kusikojulikana.
Alisema hakujua kilichoendelea baada ya kuondoka nyumbani lakini baadaye alibaini kuwa alikuwa katika Kijiji cha Olkokola wilayani Arumeru na alikwenda kwenye nyumba ya mwanamke mmoja asiyefahamiana naye akamuomba maji ya kunywa.
“Baadaye nilizinduka, nikaendelea kuishi palepale nyumbani kwa yule mama lakini sifahamu nilikuwa nafanya nini.
“Juzi ndiyo nikashangaa kujikuta nimerudi nyumbani, mimi sijui nini kilikuwa kikiendelea,” alisema binti huyo.
MAJIRANI NAO
Majirani kadhaa waliokuwepo nyumbani kwa Obed walilielezea tukio hilo kwamba ni la ushirikina huku wakisema ni jambo la kuogofya ambalo halikuwahi kutokea kijijini hapo kabla.
Wengine walisema kuwa binti huyo alifufuka na wengine walisema alichukuliwa msukule.
Mkuu wa Polisi wa Kituo cha Usa River, Benedict Mpujila amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema uchunguzi unafanyika.
KUMBUKUMBU
Mapema mwaka jana tukio la kishirikina liliibuka katika wilayani Arumeru eneo la Kwa Mrefu ambapo mtu mmoja alidaiwa kudondoka na ungo, muda mfupi baadaye alitoweka na kwenye ungo kubaki mayai na kuku mweupe.