Friday, May 16, 2014

VICKY KAMATA KUFUNGA NDOA YENYE BAJETI YA SHILINGI MILIONI 96 HIVI KARIBUNI

HAYAWI…hayawi sasa yamekuwa! Habari ya mjini ni maandalizi kabambe ya harusi ya staa wa Bongo Fleva na Mbunge wa Viti Maalum (CCM) anayewakilisha Vijana Mkoa wa Geita, Vicky Pascal Kamata ikidaiwa kuwa shughuli hiyo itatafuna kiasi cha Sh. milioni 96, Ijumaa lina mkanda kamili.

IJUMAA LAMNASA BWANA HARUSI Habari kutoka kwa chanzo cha ndani zilisema kuwa Vicky anatarajia kufunga pingu za maisha Mei 24, mwaka huu na mchumba wake wa muda mrefu ambaye Ijumaa limemnasa aliyejulikana kwa jina la Charles Pai. Ilidaiwa kwamba mwanaume huyo ni kigogo ndani ya kampuni moja ya huduma za simu hapa nchini.
vik2 
Staa wa Bongo Fleva na Mbunge wa Viti Maalum (CCM) anayewakilisha Vijana Mkoa wa Geita, Vicky Pascal Kamata akiwa na mchumba wake Charles Pai.

HARUSI YA REKODI Kwa mujibu wa mtonyaji wetu huyo ambaye naye ni miongoni mwa wanakamati, harusi hiyo inatarajiwa kuweka rekodi ya aina yake Bongo. “Sijawahi kuona harusi ya kifahari kama ya Vicky, itafanyika tarehe 24 mwezi huu, ina siku chache tu, huwezi kuamini mambo yote yamekamilika,” alisema mpashaji wetu.

HOTELI YA NYOTA TANO Imesemekana kwamba baada ya ndoa hiyo kufungwa kanisani, shughuli itahamia katika hoteli yenye hadhi ya nyota tano ya Hyatt Regency, The Kilimanjaro iliyopo Posta, Dar ambapo waalikwa watagonga mnuso wa maana na vinywaji vya kumwaga.

Habari zilieleza kuwa sherehe hiyo itahudhuriwa na mawaziri, wabunge wenzake, vigogo mbalimbali serikalini na baadhi ya wasanii wenzake. Ilidaiwa kuwa bajeti ya shughuli hiyo imefikia kiasi hicho kwani Vicky anataka iwe ya aina yake.
vik

BAJETI MIL. 96 Kwa mujibu wa mwanakamati huyo, kwa bajeti hiyo ya Sh. milioni 96, Vicky atakuwa amevunja rekodi ya ndoa za mastaa zilizowahi kufungwa Bongo.

“Nakwambia harusi ya Vicky haina mfano, itafunika harusi za vigogo na mastaa wengi, itakuwa ya aina yake. Bajeti yake siyo ya kitoto. “Watu wengi wamemchangia, achilia mbali na kuweka hela yake yeye binafsi na mchumba wake, kitu kama Sh. milioni 40.

KUVUNJA UKIMYA NA UVUMI “Hakika mheshimiwa amejipanga kuvunja ukimya na uvumi mwingi juu ya maisha yake ya kisiasa na jamii inayomzunguka,” alisema mtoa habari wetu na kuongeza:

VIKAO NI DAR, DODOMA “Huwezi kuamini, vikao vingi vya harusi sisi wanakamati tunafanyia Dar. Lakini mara nyingine tunafanyia Dodoma kwa sababu waheshimiwa wengi wanakamati wako huko.

“Hata kwenye vikao watu wanakunywa na kula je, siku yenyewe itakuwaje? Unaambiwa msafara wa magari ya kifahari tupu na utakuwa kama wa rais ukiongozwa na farasi.

VICKY ANASEMAJE? Baada ya kupata habari hizo, gazeti hili lilimsaka Vicky kwa udi na uvumba ili kujua mchakato mzima wa harusi umekaaje lakini simu yake ya mkononi iliita bila kupokelewa huenda ni kwa sababu ya kubanwa na vikao vya Bunge la Bajeti vinavyoendelea mjini Dodoma huku bwana harusi akishindwa kutoa ushirikiano.

Hata hivyo, bado tunaendelea kumsaka Vicky au kama atasoma habari hii tunaamini anaweza kupiga simu kwenye chumba cha habari na kufafanua jambo lolote juu ya tukio hilo la kihistoria katika maisha yake.