Wananchi wanaopata huduma za afya katika kituo cha afya Murongo wilayani Kyerwa mkoani Kagera, wameuomba uongozi wa kituo hicho kujenga chumba cha kuhifadhia maiti ili kuwaondolea adha wananchi wanayokumbana nayo baada ya kushuhudia maiti zikilazwa kwenye vitanda vya wagonjwa.
Wakizungumza na paparazi jana, wananchi hao walisema kuwa kutokana na kituo hicho kutokuwa na chumba cha kuhifadhia maiti wameiomba bodi ya afya ili kusaidia ujenzi wa chumba cha kuhifadhia maiti, kuondoa adha wanayokumbana nayo ya kushuhudia maiti zikilazwa kwenye vitanda vya wagonjwa.
Mmoja wa wananchi hao, Sebastiani Katunzi alisema wanapopata msiba katika hospitali hiyo wanakumbana na changamoto nyingi, kwani maiti zinalazwa kwenye vitanda vya wagonjwa jambo linalowatia wasiwasi wagonjwa waliopo wodini.
“Tumeiomba bodi ya afya wilayani hapa isaidie kujenga chumba cha kuhifadhia maiti, kwani watu tunapopata misiba tunakuwa na wasiwasi, kwani tunashuhudia maiti zikilazwa kwenye vitanda vya wagonjwa jambo ambalo siyo jema,” alisema Katunzi
Mganga Mkuu wa kituo hicho, Alobogasti Nkabyemanyira alisema kituo hicho cha afya Morongo tangu kianzishwe wagonjwa waliokuwa wanalazwa walikuwa ni wachache, hivyo ingetokea mgonjwa akafariki alikuwa anasafirishwa siku hiyo.
Nkabyemanyira alikiri kuwapo kwa tatizo hilo la kutokuwa na chumba cha kuhifadhia maiti na kueleza kwamba wagonjwa wameongezeka kiasi kikubwa na kusababisha kuwapo kwa upungufu wa vitanda pia.
“Ni kweli kuna tatizo, lakini tutawasilina na uongozi wa wilaya ili bajeti ya mwaka ujao iweze kukidhi mahitaji kama hayo,” alisema Dk Nkabyemanyira.