Wednesday, July 16, 2014

TRAFIKI WA KIKE ATEKWA NA DEREVA BAADA YA MSUKOSUKO ...

Alexander Msowoya (35), ambaye ni mkazi
wa Chang'ombe, jijini Dar es Salaam,
amefikishwa katika Mahakama ya Mwanzo
Magomeni akikabiliwa na shtaka la kumteka
nyara askari wa kike wa usalama
barabarani.
Akiwa anaendesha gari, mshtakiwa huyo
anadaiwa kumteka Kostebo Ester katikati ya
maeneo ya Tameke na Chang'ombe kabla ya

kukamatwa maeneo ya katikati ya Mabibo
na Ubungo baada ya msako mkali wa polisi
waliokuwa wakitumia redio za upepo.
Hati ya mashtaka iliyosomwa mbele ya
hakimu Mwanaidi Ngoda ilidai kuwa Julai
11, mwaka huu, saa 9:00 alasiri, eneo la kati
ya Temeke na Chang'ombe, mshtakiwa
alimteka nyara askari polisi Konstebo Ester,
alipotakiwa kuonyesha leseni yake.
Ilidaiwa kuwa Afande Ester alimkamata
mshtakiwa huyo akiwa anaendesha gari
lenye namba za usajili T 495 BKJ na
kumtaka aonyeshe leseni yake, lakini
hakufanya hivyo.
Baada ya hapo, ikadaiwa kuwa trafiki huyo
wa kike akamwamuru dereva huyo
aliyekuwa anaendesha gari aina ya Rav4 ya
rangi ya bluu kuweka gari lake pembeni,
lakini alikaidi kwa kudai ana haraka.
Kutokana na hali hiyo, ilidaiwa kuwa askari
aliingia ndani ya gari kwa kupitia
 kwenye
mlango wa nyuma na kuamuru waende
kwenye kituo cha polisi Chang'ombe.
Hata hivyo, ilidaiwa kuwa badala ya
kuelekea alikoelekezwa, mshtakiwa alianza
kwenda anakokujua yeye, hivyo kukiuka
amri halali ya polisi na kitendo hicho
kuhesabika kama ni utekaji nyara.
Awali, kabla ya kesi hiyo kusomwa, askari
polisi mmoja alimwambia mwandishi wa
habari hizi kuwa kilichomuokoa afande
Ester ni redio ya mawasiliano aliyokuwa
nayo, ambayo kwa kiasi kikubwa
ilifanikisha kujua walipo na wanakoelekea.
Hivyo, walikuwa wakifanya mawasiliano na
askari wengine waliokuwa maeneo
mbalimbali gari linapopita na ikasaidia
kukamatwa.
"Afande amepumzika nyumbani kwake.
Kwa sasa hali yake si nzuri ana presha
kutokana na tukio hili,"
alisema askari
mmoja wa kiume mahakamani hapo,
ambaye hakutaka kutaja jina lake.
Hata hivyo, alidokeza kuwa kuna
uwezekano mkubwa kesi hiyo ikapelekwa
kwenye mahakama za juu kutokana na
uzito wake, kwani ni ya utekaji nyara.
Mshtakiwa alikana shtaka hilo na
kupelekwa rumande. Kesi hiyo imepangwa
kuendelea tena Julai 27, mwaka huu.