Wednesday, August 27, 2014

GARI LA LULU LAIBUA MAZITO, LADAIWA NI GARI LA KIGOGO...POLISI WAMSAKA USIKU NA MCHANA

MAKUBWA! Mambo yamekuwa mambo, kadi ya gari jipya la staa wa sinema za Bongo, Elizabeth Michael Kimemeta ‘Lulu’ imeibua mazito kufuatia Jeshi la Polisi Dar es Salaam kubaini kuwa namba ya Sanduku La Posta (SLP) iliyoandikwa kwenye kadi hiyo ni Wizara ya Mambo ya Ndani Tanzania.
Gari ya staa wa sinema za Bongo, Elizabeth Michael Kimemeta ‘Lulu’ aina ya Toyota Rav 4 New Model
IMEVUJAJE?!
Hilo lilibainika baada ya gazeti dada na hili, Ijumaa toleo la Ijumaa iliyopita kuandika habari yenye kichwa kisemacho; LULU AANDIKA HISTORIA.
Katika habari hiyo, Lulu alipewa shavu kwa vile alinunua gari aina ya Toyota Rav 4 New Model kwa pesa zake mwenyewe tofauti na baadhi ya mastaa wa Bongo ambao huhongwa magari na wanaume.
SIMU YAPIGWA
Wakati gazeti hilo likiwa mitaani, mtu mmoja aliyedai kuwa ni afisa wa jeshi la polisi jijini Dar es Salaam alipiga simu kwenye chumba cha habari cha Global Publishers na kusema kuwa S.L.P ya 9140 iliyotumika kwenye kadi ya gari la Lulu ni ya jeshi hilo.
NI KOSA LA JINAI
Ofisa huyo aliliambia gazeti hili kuwa raia wa kawaida haruhusiwi kutumia sanduku la barua la jeshi kitu alichodai kinaonesha jinai ilifanyika wakati wa usajili ya gari hilo.
“Haiwezekani Lulu atumie Postal Office Box (P.O.Box au S.L.P) ya jeshi kwenye kadi ya gari lake ikizingatiwa kuwa yeye ni raia wa kawaida.
'Lulu’ akipozi.
“Ukiachana na hilo hata sisi maofisa wa jeshi la polisi hatuwezi kuitumia hiyo anuani kwa shughuli zetu binafsi labda kuwe na kibali maalum,” alisema afisa huyo ambaye aliomba hifadhi ya jina lake kwa vile yeye si msemaji wa jeshi hilo.
LULU ANASEMAJE?
Baada ya kupata maelezo hayo, gazeti hili lilimtafuta Lulu ili kujibu madai hayo yenye utata ambapo alisema kuna mtu alimtengenezea namba yake ya TIN (Taxpayer Identification Number) ndiye aliyemwekea anuani hiyo bila yeye kujua.
Huku akisita kumtaja kwa jina mtu huyo lakini akimtaja kwa cheo ambacho kiko wazi na mapaparazi wetu wakamjua, Lulu alifunguka hivi:
“Namiliki gari langu kihalali kabisa na nina kila kitu, niko tayari kwenda kokote kuonesha uhalali wa umiliki wangu. Kuhusu hiyo anuani, mtu aliyenitengenezea TIN Number ili nipate leseni ya udereva ndiye aliyetumia hiyo anuani, mimi sijui chochote jamani.”
AOMBA AHIFADHIWE SIRI
Katika hali ya kushangaza, Lulu aliwaambia mapaparazi wetu wasimtaje jina gazetini mtu huyo aliyemsajilia TIN akisema asitiriwe siri yake.
Kadi ya gari la ‘Lulu’ yenye anuani za jeshi la Polisi (S.L.P ya 9140).
POLISI NAO WANENA
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, ambako ndiko usajili wa gari hili ulifanyika katika ofisi za TRA, Zakaria Sebastian, alisema jeshi lake halina taarifa za kuwepo kwa jambo hilo lakini watalifuatilia kwa karibu.
“Huenda ni mke wa askari au mwanafamilia. Unajua kuna baadhi ya maofisa wana msamaha, huenda alitumia hivyo, lakini tutafuatilia,” alisema kamanda huyo ambaye alielezwa kuwa, Lulu hajawahi kuwa mke wala mwanafamilia ya mwajiriwa wa jeshi la polisi.
“Kama hajawahi kuwa mwenye kustahili kutumia anuani hii, basi tutafuatilia ili kujua wakati akiitumia, je alikuwa anakusudia kufanya jinai? Tukijiridhisha hivyo bila shaka sheria itafuata mkondo wake.”
UCHUNGUZI WA RISASI MCHANGANYIKO
Katika uchunguzi wa gazeti hili, anuani hiyo imeshatumika na Jeshi la Polisi Magomeni na Mkoa wa Polisi wa Ilala jijini Dar. Namba hiyo inatofautiana tarakimu moja na ya Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.